UN - mji wa Aleppo huenda ukawa" kaburi kubwa la pamoja"
1 Desemba 2016Tamko hilo lilitolewa saa chache baada ya watu 45 kuawa, walipokuwa wakijaribu kutoroka eneo hilo linalodhibitiwa na waasi na ambalo limeendelea kushambuliwa na vikosi vya serikali. Wakaazi wa Mji wa Aleppo wamezingirwa na vikosi hivyo vya serikali kwa karibu siku 150 bila ya kuwepo msaada wowote.Tangu siku ya jumamosi wiki hii watu elfu 25 wameyakimbia makazi yao baada ya kushamiri mapigano na kuongezeka mashambulizi ya angani.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mtaifa anayesimamia Masuala ya kibinadamu ambaye pia ni mratibu wa misaada ya dharura katika Umoja wa Mataifa Stephen O' Brien ameliomba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutafuta suluhusho la kisiasa ili kuwapa matumaini maelfu ya raia wanaotazamiwa kukimbia Aleppo."Hii leo, kutokana na matokeo ya mabomu na makombora, hospitali zote zimepigwa moja kwa moja mara nyingi na hakuna hospitali inayofanya kazi mashariki mwa mji wa Aleppo kasoro tu kitengo cha ushauri. Na vituo vingine vya afya vinafanya kazi chini ya uwezo na havina uwezo wa kutibu watu wengi, watu wengi waliojeruhiwa hawapati matibabu ya msingi. Ikiwa yapo, machache, magari ya kubebe wagonjwa, tunapokea taarifa za raia waliojeruhiwa wanakimbizwa vituo vya afya kwa kubebwa katika magari ya kuebebea mboga."
Vifo vya jana Jumatano ni vya pili katika tukio sawia na hilo katika muda usiofika saa 24 ,na vilitokea wakati raia wakijaribu kuvuka na kuingia eneo linalosimamiwa na serikali ya Syria, kupitia Jubb-al Qubba. Shirika linalochunguza masuala ya haki za binadamu nchini Syria limesema miongoni mwa waliouwa ni watoto.
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura, ameongeza kuwa wasiwasi uliopo hasa ni kwa wanaotoroka mapigano hayo."Tumepokea ripoti za kuaminika zinazoonyesha kwamba katika kesi nyingi makundi ya upinzani wamekuwa kweli wakizuia raia kutoka katika maeneo wanayoyadhibiti. Pia kuna wasiwasi kwamba ili kuyafikia maeneo yanayodhibitiwa na serikali au na majeshi ya Syria, raia wanaodhaniwa kuwa na uhusiano au uhusiano na makundi ya upinzani yenye silaha wanaweza kuwa wamewekwa kizuizini." Mataifa kadhaa wanachama wa baraza hilo la umoja wa mataifa yametaka kupitishwa azimio la kusitishwa mapigano Aleppo kwa siku 10 ili kuruhusu kuingizwa misaada ya kiutu.Urusi imelaumiwa kwa baraza hilo kutoweza kusitisha mapigano hayo. Hata hivyo balozi wa Urusi katika Umoja wa mataifa Vitaly Churkin amesema mataifa ya magharibi yanatumia maswala ya misaada ya kiutu ili kuendeleza ajenda zao za kisiasa kulazimisha mabadiliko ya utawala nchini Syria.
Mwandishi:Jane Nyingi/DPAE/AP
Mhariri: Gakuba Daniel