Mji wa Bandari wa Kismayo mikononi mwa Madobe
10 Juni 2013Mapigano makali yalizuka tangu ijumaa baada ya kundi la wanamgambo wanaomuunga mkono mbabe wa kivita Ahmed Madobe aliyejiteua binafsi hivi karibuni kuwa rais wa jimbo la kusini la Jubaland,kupambana dhidi ya wanamgambo wanaomtii kiongozi mwingine anayedai pia kuwa rais wa jimbo hilo,Hassan Basto.
Watu 18 mpaka sasa wameshapoteza maisha kufuatia vita hivyo. Kwa mujibu wa wakaazi wa Kismayo hali kwa wakati huu imetulia na sehemu nyingi za mji huo wa bandari zinashikiliwa na wapiganaji wa Madobe.Wanamgambo wa kundi hasimu wanadaiwa kutoroka lakini hawako mbali mno na mji huo.
Nani mmiliki himaya ya Kismayo?
Makundi kadhaa yanadai umiliki wa himaya ya mji wa Kismayo,mji ambao ni ngome ya zamani ya kundi linalofungamanishwa na mtandao wa alqaeda la Alshabab,na ambako sasa wanajeshi wa Kenya wanaopigana chini ya mwavuli wa Umoja wa Afrika wamekita kambi.Kikosi hicho cha Kenya kilichoingia Somalia mwaka 2011 kinaunga mkono hatua ya madobe ya kuudhibiti mji huo wa Bandari pamoja na kwamba cheo cha mbabe huyo wa kivita cha urais alichojitwika mwenyewe pamoja na jimbo la Jubaland ni vitu visivyotambuliwi na serikali kuu ya Somalia mjini Mogadishu.
Jimbo hilo la Jubaland linakutikana kusini mwa Somalia na linapakana na Kenya na Ethiopia na linadhibitiwa na makundi mbali mbali ikiwemo ya kikoo,Alshabab,wanajeshi wa Kenya na Ethiopia.Jubaland limejiunga na majimbo mengine yaliyojitangazia uhuru wake na kujitenga na nchi hiyo ya upembe wa Afrika iliyogawika,majimbo hayo ni pamoja na Puntland iliyoko kaskazini mashariki ambayo inadai kujitenga ndani ya shirikisho la majimbo huku Somaliland iliyoko kaskazini magharibi ikitetea uhuru iliojitangazia .
Rais Mohamud ataka amani
Rais wa serikali kuu ya somalia mjini Mogadishu Hassan Sheikh Mohamud amezitolea mwito pande zote zinapigana katika mji huo wa Kismayo kukomesha vita mara moja akisema enzi za mapigano zimemalizika na sasa ni wakati wa kushikamana na kutafuta njia za kuzimaliza tofauti za wasomali kwa njia ya amani na utulivu.Amesema wasomali wanapaswa kuungana na kupambana dhidi ya kundi la l-shababab.
Itakumbukwa kwamba mapigano ya Kismayo yanakuja baada ya marais wa Kenya na Somalia kukutana wiki iliyopita na kujadiliana kuhusu dhima ya Kenya katika jimbo la Jubalanda ambako kuna utajiri mkubwa wa viwanda vya mkaa,ardhi yenye rotuba na uwezekano mkubwa wa rasilimali ya mafuta katika pwani yake pamoja na gesi.Serikali ya Kenya inaliangalia jimbo hilo kama sehemu muhimu ya usalama katika kuilinda mipaka yake lakini serikali hiyo imeishia kumuunga mkono mbabe wa kivita katika Jubaland ambaye anaipinga serikali kuu ya Somalia.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed AbdulRahman