1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha ugaidi chaendelea kukwamisha shughuli Brussels

Admin.WagnerD23 Novemba 2015

Wanajeshi wanaendelea kushika doria katika mitaa ya mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels kwa siku ya tatu mfululizo huku shughuli za kawaida katika mji huo zikikwama kutokana na kitisho cha mashambulizi ya kigaidi.

Picha: picture-alliance/landov/Z. Lei

Hayo yanajiri wakati waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na rais Francois Hollande wa Ufaransa wakikutana kuzungumzia mkakati wa mashambulizi ya anga dhidi ya kundi la IS nchini Syria.

Leo ni siku ya kumi ya msako dhidi ya mmoja wa washukiwa wa mashambulizi ya Paris yaliyotokea tarehe 13 mwezi huu. Raia wa Ubelgiji Salah Abdeslam bado hajapatikana licha ya misako 19 na kukamatwa kwa watu 16.

Maafisa wa usalama bado wanaonya kuna kitisho kikubwa cha mashambulizi ya kigaidi mjini Brussels kama yale yaliofanyika katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris na kuwaua watu 130 na kuwajeruhi wengine 350.

Ubelgiji yahofia mashambulizi makubwa

Usafiri wa treni, makumbusho, shule, vyuo vikuu, majengo ya umma, maduka kadhaa na kumbi za starehe zimesalia kufungwa kwa siku ya tatu mfululizo katika mji huo wa Brussels yalipo makao makuu ya Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya NATO huku takriban maafisa 1,000 wa usalama wakishika doria katika mitaa ya Brussels.

Wanajeshi wanashika doria BrusselsPicha: Reuters/Y. Boudlal

Umoja wa Ulaya na NATO zimesema zimeimarisha usalama katika majengo yao na kuwataka wafanyakazi wao wasio fanya majukumu muhimu kutekeleza majukumu yao kutoka majumbani mwao.

Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel amesema mji huo wenye wakaazi milioni 1.2 utasalia kuwekwa katika kiwango cha nne cha tahadhari za kiusalama, hiyo ikimaanisha kuna kitisho kikubwa cha kufanyika mashambulizi makubwa ya kigaidi.

Huku hayo yakijiri, Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron akiandamana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande, wameuzuru ukumbi wa Bataclan kutoa heshima zao kwa waathiriwa wa mashambulizi ya Paris.

Ukumbi huo ulioshambuliwa na magaidi na kiasi ya watu 90 kuuawa katika msururu wa mashambulizi ambayo wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS walidai kuhusika.

Cameron amesema anaamini kuwa nchi yake inapaswa kufanya mashambulizi ya angani wakishirikiana na Ufaransa na nchi nyingine washirika nchini Syria katika juhudi za kulitokomeza kundi la IS.

Cameron aitaka Uingereza kuishambulia IS

Waziri huyo mkuu wa Uingereza amesema baadaye wiki hii, atatafuta ridhaa ya bunge la nchi yake kuidhinisha mkakati huo wa vita dhidi ya IS. Cameron ameongeza kuwa ataimarisha juhudi za kupeana taarifa za kijasusi kati ya Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande na Waziri mkuu wa Uingereza David CameronPicha: Getty Images/AFP/S. de Sakutin

Kwa upande wake, Hollande amesema Ufaransa inapanga kuongeza mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za wanamgambo wa IS nchini Syria.

Kiongozi huyo wa Ufaransa wiki hii anatarajiwa kutafuta ushirikiano zaidi kutoka viongozi wengine katika mapambano dhidi ya IS baada ya mashambulizi ya Paris.

Baada ya kukutana na Cameron, anatarajiwa wiki hii pia kuelekea Washington kufanya mazungumzo na Rais wa Marekani Barack Obama na kwenda Moscow kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW