Mji wa Dresden upo katika tahadhari kuu ya mafuriko
18 Septemba 2024Mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Dresden upo katika hatari ya kukabiliwa na mafuriko baada ya siku kadhaa za mvua kubwa zilizosababisha mafuriko katika maeneo mengi ya Ulaya ya Kati.
Kiwango cha maji katika Mto Elbe unaopitia mji huo wa Dresden, kimeongezeka kufikia mita 6 hali iliyoilazimisha serikali kutangaza onyo la pili kubwa la kutokea kwa mafuriko. Hii inamaanisha maeneo ya makaazi, barabara kuu, na barabara za reli zipo katika hatari hiyo ya kuzidiwa kwa maji.
Soma pia:Watu 18 wafariki dunia kutokana na mafuriko barani Ulaya
Katika kituo cha Schöna Gauging karibu na mpaka wa Jamhuri ya Czech kiwango cha maji ya mto huo kilifikia mita 6.56 mapema hii leo asubuhi. Viwango hivyo vinatarajiwa kuendelea kupanda kabla ya kushuka wakati wa usiku.
Hata hivyo, serikali haiamini kiwango hicho cha maji kitapita mita 7 ambayo huenda ikasababisha tahadhari kubwa zaidi kutolewa.