1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya serikali nchini Iraq vyaukomboa mji Ramadi

Mjahida29 Desemba 2015

Serikali ya Iraq imeukomboa kikamilifu mji wa Ramadi kutoka kwa wanamgambo wa dola la Kiislamu na kupeperusha bendera ya nchi hiyo katika majengo ya serikali baada ya kupata ushindi huo mkubwa.

Irak Rückeroberung von Ramadi
Mmoja wanajeshi wa Iraq akisherehekea ushindi wa kuukomboa mji wa RamadiPicha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Wapiganaji waliobeba bunduki walisherehekea kwa kucheza katika mji huo ulioko mkoani Anbar huku makamanda wakuu wakifanya gwaride barabarani baada ya kuudhibiti tena mji huo uliotwaliwa na wanamgambo wa IS mnamo mwezi Mei.

Wapiganaji hao wa jihadi wameupoteza mji wa Ramadi siku kadhaa baada ya kupoteza eneo muhimu kwenye mto Euphrates nchini Syria kwa muungano wa wakurdi na waasi wa kiarabu.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq Haider al Abadi amewapongeza wapinaji waliyoukomboa mji wa Ramadi na kuapa kuukomboa mji mwengine wa Mosul pamoja na kuwaondoa wapiganaji wa IS nchini humo ifikapo mwaka wa 2016.

Aidha Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu, uliyounga mkono mapigano dhidi ya kundi hilo kwa kutoa mafunzo pamoja na silaha kwa jeshi la Iraq na pia kulisaidia kupitia mashambulizi yake ya angani katika ngome za IS, umewapongeza pia wanajeshi wa Iraq kwa kuukomboa mji wa Ramadi.

Waziri Mkuu wa Iraq Haider Al AbadiPicha: picture-alliance/dpa/E. Laurent

Kukombolewa kwa mji wa Ramadi kwapongezwa

Naye Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameliita tukio hilo la ukombozi ushindi mkubwa dhidi ya wapiganaji hao wa jihadi huku Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akisema hii inaonesha kwa mara nyengine tena kuwa kundi hilo linaweza kushindwa.

Iraq hata hivyo haijatoa idadi yoyote ya wahanga kwa vikosi vya serikali lakini ripoti ya maafisa wa afya inasema takriban wapiganaji wa serikali 100 walifikishwa katika hospitali ya Baghdad.

Maafisa wamesema wanamgambo wa IS waliwatumia raia kama ngao ya kukimbia mapigano hayo baada ya kubainika wazi kwamba wanaupoteza mji wa Ramadi.

Moja wa wanajeshi akipeperusha bendera ya Iraq baada ya ushindi wa RamadiPicha: picture-alliance/AP Photo

Wiki moja iliyopita wanamgambo hao walikadiriwa kuwa na wapiganaji 400 waliyokuwa wanapambana mjini Ramadi lakini hadi sasa haijajulikana ni wangapi hasa waliouwawa na wangapi waliyofanikiwa kutoroka.

Kwa sasa bado jeshi la Iraq halijaingia katika makao makuu ya zamani ya serikali kwa kuhofia mitego iliowekwa na IS. Kulingana na Brigedia jenerali Majid al-Fatlawi IS wameweka mabomu zaidi ya miatatu barabarani na katika majengo ya serikali.

Mwandishi: Amina AbubakarAFP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga