1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mji wa Dnipro washambuliwa vikali na Urusi

22 Mei 2023

Jeshi la Ukraine limesema vikosi vya Urusi vimeulenga mji wa mashariki wa Dnipro usiku wa kuamkia leo kwa makombora 16 na mashambulizi 20 ya droni zilizotengenezwa Iran.

Ukraine Krieg | Angriff auf Dnipro
Picha: Dnipropetrovsk Regional Military-Civil Administration/REUTERS

Kamandi ya Jeshi la Ukraine imesema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook kuwa mashambulizi hayo dhidi ya wanajeshi na miundombinu yalifanyika kwa kutumia aina mbalimbali za makombora na droni chapa ya Shahed zinazotengenezwa nchini Iran, na kuongeza kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuziharibu ndege zote 20 zisizotumia rubani pamoja na manne kati ya makombora 16, bila hata hivyo kutoa ufafanuzi.

Soma pia: Mkutano wa G7: Zelensky ashinikiza mpango wa amani Ukraine mjini Hiroshima

Dnipro ni mji mkubwa wenye wakaazi karibu milioni moja kabla ya vita, ukiwa umbali wa karibu kilomita 125 kutoka safu ya sasa ya mapigano. Maafisa wamesema ukubwa wa mashambulizi ya usiku ulikuwa hauna kifani.

Gavana wa mkoa Sergiy Lyask aliandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba vikosi vya Ukraine vilihimili mashambulizi ya ''mafashisti, magaidi na wanyama", na kuongeza kuwa jumla ya watu wanane walijeruhiwa katika mashambulizi hayo, akiwemo mwanaume mwenye umri wa miaka 25 aliejeruhiwa katika shambulizi la kombora katika wilaya moja na saba, wakiwemo wanawake wawili katika wilaya nyengine.

Wagner kuondoka Bakhmut

Wakati haya yakijiri, mkuu wa kundi la mamluki wa kijeshi la Urusi la Wagner Yevgeny Prigozhin, amesema Jumatatu kuwa vikosi vyake vitandoka Bakhmut mwishoni mwa mwezi huu na kukabidhi udhibiti wa mji huo kwa jeshi la Urusi.

"Wagner itaondoka Artemovsk kutoka Mei 25 hadi Juni 1," Yevgeny Prigozhin alisema katika rekodi ya sauti kwenye mtandao wa Telegram.

Soma pia: Zelenskiy amesema Bakhmut bado inadhibitiwa na Ukraine

Bakhmut hapo awali ilijulikana kama Artemovsk, kwa heshima ya mwanamapinduzi wa Soviet, kabla ya Ukraine kuibadili jina.

Athari za vita vya Ukraine kwa watumiaji wa ngano Afrika

02:40

This browser does not support the video element.

Prigozhin alisema mamluki hao walikuwa wameweka "safu za ulinzi" kwenye viunga vya magharibi mwa mji huo kabla ya uhamisho uliopangwa wa udhibiti kwa jeshi la Urusi.

Ukraine imesisitiza hata hivyo kuwa vikosi vyake vilikuwa vinaendelea kusonga mbele pembezoni mwa mji huo ulioharibiwa, ingawa kasi yao ya kusonga mbele ilikuwa imepungua na Urusi ikileta wanajeshi zaidi.

Urusi ilidai siku ya Jumamosi kwamba ilikuwa imeuchukuwa kikamilifu mji wa Bakhmut, lakini maafisa wa Ukraine wamesema tangu wakati huo kwamba vikosi vya Kyiv vinaendelea kudhibiti sehemu ndogo ya mji huo.

Naibu waziri wa ulinzi Hanna Malyar amekariri pia leo kuwa  Ukraine ina pia udhibiti mdogo ndani ya mji huo.

"Mapigano yanaendelea," alisema Malyar, siku moja baada ya Rais Volodymyr Zelensky kusema Bakhmut "haitekiwi" na Urusi.

Malyar alisema wanajeshi wa Kyiv wameendelea kuidhibiti wilaya ya "Ndege" ya Bakhmut.

Soma pia: Zelensky awasili Japan kwa mazungumzo na viongozi wa G7

"Vita vya miinuko mikubwa kwenye ubavu -- kaskazini na kusini mwa vitongoji -- vinaendelea," aliongeza.

NATO yajadili jinsi ya kuipatia Ukraine silaha zaidi

01:30

This browser does not support the video element.

Kiwanda cha nyuklia Zaporizhzhya chakatiwa tena umeme

Mkuu wa shirika la nishati ya atomiki la Umoja wa Mataifa, IAEA, Rafael Grossi, amesema Jumatatu kuwa mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhya umekatwa kabisaa kutoka kwenye ugavi wa nje wa umeme, hali ambayo amesema inauweka usalama wa nyuklia kiwandani hapo katika hatari kubwa.

Kampuni ya nyuklia ya Ukraine Enerhoatom imethibitisha tukio hilo kwenye kiwanda hicho kinachokaliwa na wanajeshi wa Urusi kusini mwa Ukraine, ikisema Jumatatu asubuhi kuwa kiwanda hicho kiliharibiwa kwa shambulio.

Hata hivyo Ukraine imesema kuwa tayari imekiunganisha tena kiwanda hicho kwenye ugavi wa nje wa umeme.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW