Hali halisi ya mfumo wa kuishi pamoja Ujerumani
2 Juni 2022Mjongeleano wa jamii za watu wa tamaduni mbali mbali nchini Ujerumani ni suala muhimu linalotajwa kupewa kipaumbele. Na kwahakika inaelezwa kwamba Ujerumani milango iko wazi kwa kila mtu anayeonesha uwezo kiutendaji na bidii. Na hilo ni jambo zuri kabisa, lakini ukweli ni kwamba hali halisi haiko hivyo. Ripoti ifuatayo iliyoandikwa na Insa Wrede inaangazia kuhusu hali ilivyo.
Nchini Ujerumani, mtu anayetokea katika mazingira bora ndiye anayepewa nafasi. Mara nyingi hali inaonesha kipaji na bidii havitoshi kumfanya mtu kupewa nafasi.
Watu wanapaswa pia kuelewa kuna mambo yaliyojificha yanayotumiwa na wenye mamlaka, kwa mfano mtu anapaswa kufahamu kuna namna ya mtu unavyotakiwa kuishi, aina ya mavazi unayovaa, unatakiwa ufahamu mambo gani ya kujishughulisha nayo katika wakati usiokuwa wa kazi na pia lugha unayotumia kuzungumza. Yote hayo utabidi kuyazingatia kabla ya kufunguliwa milango ya fursa katika nchi hii.
Kwa maneno mengine ni kusema mazingira ya maisha yako na ulikotokea yana mchango mkubwa unaoweza kuamua juu ya mwelekeo wako kielimu na katika fursa za kitaaluma unazoweza kupata nchini Ujerumani na kwa kiasi gani unaweza kukumbana na ubaguzi. Kilichowazi kabisa ni kwamba nchini Ujerumani,ubaguzi unaanza katika ngazi za awali kabisa.
Zaidi ya asilimia 80 ya watoto wanaotokea kwenye familia za waliosoma ndio wanaoingia kwenye shule zinazojulikana kama Gymnasium.
Na idadi ya watoto kutoka familia za watu wenye elimu ya kawaida haifiki hata nusu anasema mwandishi habari Konstantina Vassiliou-Enz ambaye pia ni mmoja wa waanzilishi wanaotoa ushauri katika harakati za kuleta mjongeleano zaidi wa jamii za watu wa tamaduni mbali mbali katika vyombo vya habari.Na mara nyingi pia hatma ya mwelekeo wa kielimu ya mtoto inafungamanishwa na elimu ya wazazi wake.
Kwa mfano vijana 79 kati ya 100 wanaotokea kwenye familia za wasomi hujikuta moja kwa moja wanafanikiwa kuanza elimu ya chuo kikuu wakati kwa familia za walio na elimu ndogo ni watoto 27 kati ya 100 ndio wanaoweza kupata fursa hiyo.
Lakini mbali na suala la elimu ya wazazi kuna pia masuala mengine kama vile uwezo wa wazazi kiuchumi mfano ni ikiwa wazazi wanajiweza au wanafanya kazi yote hayo yanamchango.
Na mambo huwa ni mabaya zaidi kwa wale wanaotokea kwenye familia za chini mara nyingi hujikuta wakibaguliwa kutokana na mazingira waliyoko,kwa mfani ikiwa wanatokea katika familia za wageni.
Vassiliou-Enz anasema ni wazi kwamba nchini Ujerumani kipato cha wazazi na kiwango cha elimu yao ni mambo muhimu sana yanayozingatiwa katika mafanikio ya kielimu ya mtoto na mara nyingi watoto wenye asili ya kigeni mara nyingi wanatokea kwenye familia za wenye kipato kidogo.Aidha sio siri kwamba nchini Ujerumani watu wanaotokea katika familia zenye uwezo na elimu ndio wanaopewa kipaumbele cha kupata nafasi kwenye mafunzo ya vitendo kwenye taasisi mbali mbali.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef