Mjue Rais mpya wa Ujerumani: Frank- Walter Steimeier
12 Februari 2017Frank-Walter Steinmeier amechaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani. Mfuasi huyo wa chama cha Social Democratic SPD ameingia katika uwanja wa kisiasa kwa karibu ya miaka 20 sasa. Miaka michache iliyopita aligombea kiti cha kansela na kushindwa na Angela Merkel. Baada ya kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje mara mbili, Frank-Walter Steinmeier sasa amefikia kileleni mwa jukumu lake kama mwanasiasa:Raisi wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani.
Hakuna aliyekuwa akishuku juu ya uwezekano wa kuchaguiliwa kwake kwasababu Frank-Walter Steinemeier alikuwa mgombea aliyependekezwa kwa pamoja na vyama shirika katika serikali kuu ya muungano, CDU, CSU na SPD. Kwa kumteuwa yeye, vyama ndugu cha Christian Democratic Union na Christian Social Union vimesababisha mwanasiasa huyo wa SPD kufika kileleni mwa wadhifa wa kisiasa nchini Ujerumani.
Tayari Steinemeier ni gwiji katika viwanja vya kisiasa nchini Ujerumani,hadi hivi karibuni yeye ndie aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa serikali kuu ya muungano ya vyama vya CDU/CSU na SPD. Utafiti wa maoni ya wananchi umebainisha kwamba wajerumani waalio wengi walikuwa wakimwangalia Steinemeier kuwa ndio wajihi wa diplomasia ya Ujerumani.
Wadhifa wake kama waziri wa mambo ya nchi za nje ulikuwa daraja ya mwisho kati ya daraja kadhaa alaizopanda mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 60, katika kipindi cha takriban miaka 20 cha maisha yake ya kisiasa. Waziri katika ofisi ya kansela,mwenyekiti wa kundi la wabunge wa SPD katika bunge la shirikisho,waziri wa mambo ya nchi za nje na mgombea kitti cha kansela. Kwa hivyo Frank-Walter Steinmeier, si mgeni anaposhika nafasi inayoachwa na Joachim Gauck kama rais wa shirikisho.
Kinyume kabisa Steinmeier anaweza kufanya mengi mazuri akiwa rais wa shirikisho.Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nchi za nje anasifiwa na vyote vyote, ana uzoefu katika uwanja wa kidiplomasia, anathaminiwa kimataifa na kipaji katika kusaka ufumbuzi mizozo inapotokea.Utafiti wa maoni umedhihirisha anashikilia nafasi ya mbele miongoni mwa wanasiasa wanaopendwa zaidi na wananchi humu nchini. Na pengine sifa hii ya kuangaliwa kama kipenzi cha umma ndio sababu kuu ya kuchaguliwa mgombea huyo wa chama cha SPD kuwa rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani.
Wadadisi wamekuwa kwa miaka sasa wakizungumzia juu ya kiu cha muda mrefu cha mtoto huyo wa Saramala kutoka jimbo la North Rhine Westphalia cha kutaka kukabidhiwa wadhifa huo wa juu kabisa.
Hadhi ya urais ilionekana mapema.
Na katika ziara zake kadhaa kama waziri wa mambo ya nchi za nje ambazo ziligonga kilomita laki nne kwa mwaka, Frank-Walter Steinmeier daima alijitokeza kwa hadhi za rais. Alikuwa makini na kuzingatia usawa na haki. Hasa katika mzozo wa Ukraine, alijipatia sifa ya kuwa mwanadiplomasia mwenye bidii ambae hakuchoka kufunga safario kila wakati kati ya Kiev na Moscow. Steinmeier alifanikiwa kupunguza makali ya mzozo huo kutokana na fasaha na jinsi anavyopima anachokisema. Ndio maana Steinmeier aliugutua ulimwengu na kugonga vichwa vya habari katika kampeni za uchaguzi za Marekani pia alipomtaja Donald Trump kuwa ni "mtu mwenye kuhubiri chuki."Baadae alisema kuchaguliwa Trump kama rais itakuwa "mwisho wa mwongozo wa kale wa nidhamu ulimwenguni."
Shughuli zake za kisiasa zilianzia na kansela wa zamani Gerhard Schröder ambapo Steinmeier alikuwa akiongoza ofisi ya Schröder alipokuwa bado waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony.Baada ya SPD kukabidhiwa jukumu la kuunda serikali mwaka 1998 mjini Berlin, Steinmeier akachaguliwa kuwav katibu wa dola na baadae waziri katika ofisi ya kansela mjini Berlin.Mwaka 2005 akachaguliwa kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje katika serikali ya muungano ya kansela Angela Merkel-wakati ule Steinmeier akakabidhiwa apia wadhifa wa makamo kansela na katika uchaguzi wa mwaka 2009 akagombea kiti cha kansela kwa tikiti ya chama chake cha SPD.
SPD walishindwa wakati ule. Mwaka 2013 Steinmeier akakabidhiwa tena wadhifa wa waziri wa mambo ya nchi za nje katika serikali mpya ya muungano ya vyama vya CDU/CSU na SPD. Baada ya Hans Dietrich Genscher wa chama cha kiliberali cha FDP Steinmeier ana sifa ya kushikilia wadhifa huo kwa muda mrefu .Amezalaiwa january 5 mwaka 1956 katika mji wa Detmold kataika jimbo la North Rhine Westphalia.Frank-Walter Steinemeier na mkewe Elke Büdenbender wana mtoto mmoja wa kike.
Mwandishi:Fuchs,Richard/Hamidou Oumilkheir
Mhariri:Josephat Charo