Mjumbe Maalum wa Marekani mashariki ya kati, Mitchell kufanya ziara ya siku moja, Israel na Palestina.
15 Aprili 2009Huu ndio ujumbe atafika nao, Israel na nchini Palestina mjumbe maalum wa Marekani kuhusiana na masuala ya mashariki ya kati, George Mitchell . Hii itakuwa ziara yake ya kwanza eneo hilo, tangu waziri mkuu wa Israel mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuingia madarakani.
Tangu alipoteuliwa mjumbe maalum wa Marekani Mashariki ya kati, Mitchell amefanya ziara mbili, katika eneo hilo. Lakini hii itakuwa ziara yake ya kwanza nchini Israel, tangu serikali ya muungano ya Benjamin Netanyahu kuingia madarakani.
Kabla ya ziara yake nchini Israel na eneo la Palestina, Mitchell alizuru nchi nyingine za kiarabu kusikiza sauti zao ili kupata mkakati muafaka wa kutatua mzozo huu wa Israel na Palestina.
Awamu ya kwanza ya ziara ya Mitchell ilikuwa nchini Algeria. Katika mkutano na rais wa Algeria Abdul Aziz Bouteflika, mjumbe huyu maalum, alisisitiza suluhu ya kudumu ya kuutanzua mzozo baina ya Palestina na Israel ni kuundwa kwa dola mbili, ya Palestina na Israel zitazoishi pamoja kwa amani. Mitchell pia alikuwa nchini Tunisia pia katika juhudi hizi za kidiplomasia Mashariki ya Kati.
Kulingana na Mitchell, utawala mpya wa rais Obama unalichukulia swala zima la amani mashariki ya kati kama faida kwa Marekani.
Nchini Israel Mitchell atafanya mkutano wake wa kwanza na waziri mkuu, Benjamin Netanyahu. Pia atakutana na rais wa Israel Shimon Peres na waziri wa ulinzi Ehud Barak. Mkutano kati ya Mitchell na Peres, mbali na swala la Israel na Palestina pia watazungumzia mbinu zipi zinafaa kuchukuliwa, kuizuia Iran isikamilishe mradi wake wa nyuklia.
Kisha Mitchell ataelekea Ramallah kwa miadi na viongozi wa Palestina, wakiongozwa na rais Mahmoud Abbas.
Baada ya kukamilisha ziara hii ya siku moja, Mitchell ataelekea nchini Misri pia kwa mazungumzo na viongozi wa huko. Misri ndio mwenyeji wa mazungumzo ya upatanishi kati ya kundi la Hamas na Fatah.
Katika mkutano mwingine na waziri wa mambo ya nje wa Morocco, mjumbe huyu maalum wa Marekani alitilia mkazo kuwa rais Obama anaunga mkono kubuniwa kwa dola mbili za Palestina na Israel zitazoishi pamoja kwa amani. Ni mkakati Obama ingawa anautilia pondo aliurithi kutoka kwa mtangulizi wake Rais George Bush.
Mwandishi: Munira Muhammad/ AFP
Mhariri:M.Abdul-Rahman