Mjumbe wa amani Libya ataka wapiganaji wa kigeni waondoke
18 Januari 2020Ghassan Salame amesema katika mahojiano na gazeti la Al-Sharq Al-Awsat yaliyochapishwa leo kuwa "tumewasilisha mpango wa usalama ambao unahitaji kuondolewa kwa wapiganaji wote wa kigeni, bila kuzingatia uraia wao."
Salame amesema kuwa kusitisha uingizaji haramu wa silaha nchini Libya pia utakuwa kwenye mada ya mazungumzo ya kesho Jumapili mjini Berlin. Kwa mujibu wa nakala ya ndani ya Umoja wa Mataifa, kongamano hilo litalenga kutafuta makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano na utekelezwaji wa marufuku iliyopo ya biashara ya silaha nchini Libya.
Mkutano wa kilele wa Berlin uliandaliwa kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, anayeongoza mazungumzo ya kutafuta suluhiso la amani kwa mzozo wa Libya pamoja na Salame.
Wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 10, akiwemo Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani Mike Pompeo na Rais wa Urusi Vladmir Putin, wanatarajiwa kuwa katika mji mkuu wa Ujerumani kwa ajili ya mazungumzo hayo ya amani yanayoandaliwa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Taarifa ya serikali ya Ujerumani imesema waziri mkuu wa serikali ya Libya inayotambulika kimataifa, Fayez al-Sarraj wa serikali ya Umoja wa Kitaifa – GNA, na kiongozi wa waasi Khalifa Haftar wa Libyan National Army – LNA wamealikwa katika mkutano wa Berlin. Haijafahamika kama watahudhuria.
Mazungumzo ya amani yaliyoandaliwa na Urusi mapema wiki hii yalikamilika bila ya Haftar kusaini makubaliano ya kusitisha vita.
Rais wa Uturuki Reccip Tayyip Erdogan leo ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa ya mjini Tripoli kuelekea mkutano wa mjini Berlin wa kutafuta amani ya Lbya.
Katika makala iliyochapishwa na tovuti ya jarida la Politico, Erdogan amesema viongozi wa Ulaya wanapaswa kupunguza maneno na badala yake wajikite kuchukua hatua madhubuti kwenye mzozo wa Libya.
Nchini Libya kwenyewe, waandamanaji watiifu kwa Jenerali mwenye nguvu nchini Libya Khalifa Haftar wamezuia shughuli za bandari muhimu inayotumika kusafirishaji mafuta.
Mapema leo waandamanaji waliizuia meli moja ya mafuta kutia nanga kwenye bandari ya Hariga iliyopo mashariki ya mji wa Tobruk.
Msemaji wa jeshi linaloongozwa na Haftar ametetea kufungwa kwa bandari hiyo na miundombinu ya uzalishaji mafuta akisema hatua hiyo imechukuliwa na raia wenyewe wa libya.