1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za kigeni zatakiwa kujiondoa kwenye mzozo wa Libya

7 Januari 2020

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salame amezitaka nchi zinazoyaunga mkono makundi yanayohasimiana nchini humo kuacha kufanya hivyo.

Italien Mittelmeerdialoge in Rom | UN-Sonderbeauftragter für Libyen Ghassan Salame
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Tarantino

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salame amezitaka nchi zinazoyaunga mkono makundi yanayohasimiana nchini humo kuacha kufanya hivyo.

Akizungumza baada ya kulihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana, Salame amesema Libya inateseka kwa kiasi kikubwa kutokana na mataifa ya kigeni kuuingilia mzozo wa nchi hiyo kwa njia tofauti.

''Silaha zinauzwa kwa Walibya, silaha zinatolewa kwa Walibya na majeshi ya kigeni yanayotafuta kuweka kambi za kudumu Libya. Aina hii ya uingiliaji wa moja kwa moja unayafanya mambo kuwa magumu zaidi. Kuna silaha za kutosha Libya, hawahitaji zaidi. Kuna mamluki wengi Libya, hivyo wacheni kupeleka mamluki wengine. Wacheni aina zote za uingiliaji wa kigeni,'' alifafanua Salame.

Uturuki yapeleka majeshi

Matamshi yake ameyatoa siku moja baada ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutangaza kuwa anapeleka wanajeshi wa nchi yake Libya. Uturuki inaiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa ya Tripoli ya Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, GNA inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiijadili LibyaPicha: picture-alliance/Xinhua News Agency/Li Muzi

Serikali hiyo inapambana na vikosi vya mashariki vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar, anayeungwa mkono na Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Urusi.

Baada ya hotuba ya Salame, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema lina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mapigano nchini Libya. Baraza hilo limerudia kuelezea haja ya kutekeleza marufuku ya kuingiza silaha Libya iliyowekwa na Umoja wa Mataifa na kuachana na kuiingilia nchi hiyo kijeshi.

Salame amesema wale waliolipigia kura azimio la marufuku ya kuingiza silaha nchini Libya wanawajibika kulitekeleza. Mjumbe huyo pia amewaambia waandishi habari kwamba jeshi la Haftar la Libyan National Army, LNA linahusika na mashambulizi yaliyotokea Jumamosi iliyopita na kuwaua watu wapatao 28.

Khalifa Haftar na Fayez al-Sarraj

Salame amesema mwezi Julai alitoa wito wa kufanyika mkutano wa kimataifa kuunga mkono juhudi za kuwaleta pamoja Walibya na kwamba ana matumaini mkutano utafanyika Berlin, Ujerumani katika wiki zijazo au ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwezi Januari

Sirte yatekwa na vikosi vya Haftar

Wakati huo huo, vikosi vitiifu kwa Jenerali Haftar vimetangaza kuutwaa mji wa Sirte. Mji huo wa pwani uliangukia mikononi mwa vikosi hivyo jana Jumatatu. Tangu mwaka 2016, Sirte umekuwa ukidhibitiwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa vikosi hivyo, Ahmed al-Mosmari ametangaza kuuteka mji wa Sirte katika mkutano na waandishi habari kwenye mji wa mashariki wa Benghazi. Al-Mosmari amesema Sirte imekombolewa na kwamba operesheni ilifanyika kwa haraka sana na ilidumu kwa muda wa saa tatu tu.

Kulingana na shirika la habari la Ufaransa, AFP, serikali ya Tripoli bado haijathibitisha taarifa hizo, lakini kamanda wa jeshi linaloiunga mkono serikali hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina amekiri kuwepo kwa taarifa hizo.

(DPA, AP)