1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Marekani arudi Mashariki ya kati kuionya Taliban

10 Agosti 2021

Mwakilishi maalum wa Marekani Zalmay Khalilzad, amerudi Mashariki ya kati leo Jumanne na kulionya kundi la Taliban kwamba lisitafute ushindi wa kivita ili kuongoza Afghanistan.

Afghanistan Friedensgepräche in Doha
Picha: Hussein Sayed/AP/dp/picture alliance

Katika ujumbe wake Khalilzad amesema iwapo Taliban itachukua madaraka kwa nguvu serikali watakayounda haitatambuliwa.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Khalilzad yupo mjini Doha, Qatar kwa mazungumzo na kundi la Taliban na anatarajiwa kuwashinikiza wanamgambo hao wasitishe mapambano yao baada ya wanamgambo hao kuiteka miji mikuu kadhaa ya mikoa.

Katika mazungumzo hayo Khalilzad anatarajia kusaidia kupatikana suluhisho la pamoja la jamii ya kimataifa juu ya hali inayoendelea kuzorota nchini Afghanistan. Soma zaidi Taliban wauteka mkoa mwingine tena Afghanistan

Haya yanajiri wakati mashambulizi ya mfululizo ya wiki moja yakiendelea, huku majeshi ya Marekani na Jumuiya ya kujihami ya NATO yakikamilisha kuondoka Afghanistan.

Taliban imekamata miji mikuu mitano kati ya 34 ya mikoa. Sasa wanapambana na Serikali inayoungwa mkono na nchi za Magharibi kudhibiti miji mengine mitatu, pamoja na mji wa Lashkar Gah, mji mkuu wamkoa wa kusini wa Helmand,  na mji mkuu katika jimbo jirani la Kandahar.

Mashambulizi yameongezeka

Zalmay KhalilzadPicha: AFP/W. Kohsar

Marekani imesema mashambulizi ya Taliban yanaongezeka, na yanasababisha vifo na kuwajeruhi wengine katika vita hivyo.

Mwakilishi maalum wa Marekani Zalmay Khalilzad ameelezea wasiwasi mkubwa juu ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Afghanistan.

Khalilzad amedokeza kuwa serikali ya Afghanistan na wanamgambo wa Taliban bado wako mbali katika kufikia makubaliano ya amani. 

Wakati huo huo nchi sita wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetuma barua kwa umoja huo kuonya dhidi ya marufuku ya kuwatimua waomba hifadhi kutoka Afghanistan ambao maombi yao yanakataliwa. Soma zaidi Raia wa Afghanistan waliofanya kazi na Marekani wahamishwa

Kupitia mtandao wa twitter Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Sammy Mahdi amesema kwamba kama baadhi ya maeneo ya nchi hiyo hayako salama haimaniishi kila nchi inalazimika kuwapatia ulinzi Waafghanistan.

Ujerumani, Austria, Uholanzi, Denmark na Ugiriki yapo pamoja na Ubelgiji katika hoja walioyoituma kwa Umoja wa Ulaya.

Suala hilo linatarajiwa kujitokeza katika mkutano utakafanyika mtandaoni wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya wa maswala ya ndani mnamo Agosti 18, ambayo ulipangwa hasa kujadili kuongezeka kwa uvukaji haramu  wa mipaka kutoka Belarus kwa nchi mwanachama wa umoja huo Lithuania.

 

Vyanzo:AP/Reuters/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW