1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Marekani kwa Afghanistan ajiuzulu

19 Oktoba 2021

Mjumbe maalumu wa Marekani kwa Afghanistan, Zalmay Khalilzad ametangaza kujiondoa katika wadhfa wake kufuatia kile kinachoelezwa namna mbaya ya Marekani katika kujiondoa kwake nchini Afghanistan.

USA Sondergesandter für Afghanistan Zalmay Khalilzad
Picha: Rod Lamkey/CNP/MediaPunch/imago images

Anakosolewa kwa kutofanikisha shinikizo la kutosha la mazungumzo ya amani kwa kundi la Taliban pale yalipoanza wakati utawala wa Rais Donald Trump, lakini Waziri wa Mambo ya Nje Anthony Blinken amemshukuru kwa kazi yake. Katika pongezi zake hizo kwa balozi huyo wa zamani wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa na Afghanistan alisema anatanguliza shukrani zake kwa miongo kadhaa ya kuwahudumia Wamarekani.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Zalmay Khalilzad atakuwa kando ya kiti chake juma hili, baada ya kuhudumu nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu katika tawala zote za Trump na Biden. Na tayari kiti chake atakikalia, Thomas West.

Khalilzad aliwahi kutaka kuachia ngazi mapema Mei.

Mjumbe wa Taliban Shahabuddin Delawar Picha: Stringer/REUTERS

Awali Khalilizad alipanga kung'atuka katika wadhfa huo mwezi Mei baada ya Rais Biden kutangaza kuyaondoa kabisa majeshi ya Marekani kabla ya kumbukumbu ya miaka 20 mashambulizi ya 9/11, lakini aliombwa asalie na akanafanya hivyo.

Kimsingi Khalilzad amekuwa akihudumu kama mjumbe maalumu wa upatanishi katika tawala za Trump na Biden tangu Septemba 2018, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo Mike Pompeo kumpa nafasi ya kuongoza timu ya usuluhishi kati ya serikali ya Afghanistan na wanamgambo wa Taliban.

Kushindwa kwa upatanishi wa Taliban na serikali ya Afghanistan.

Khalilzad mwenye asili ya Afghanistan alishindwa kuziweka pamoja pande hizo mbili, kwa msingi wa mgawanyo wa madaraka lakini alifanikisha mjadala mkubwa kati ya Marekani na Taliban mwezi Feburuari 2020, ambao ulizaa matunda ya kuifikisha mwisho vita vya muda mrefu kabisa vya Marekani nchini Afghanistan.

Makubaliano hayo na Taliban, yanatazamwa kama mzizi wa utawala wa Biden kuviondoa vikosi vyote vya Marekani nchini Afghanistan, hatua ambayo wengi wana amini ilifanywa kwa kuharakishwa na pasipo kuwa na mpango wa kutosha. Katika operesheni hiyo maelfu ya raia wa Afghanistan ambao walikuwa wakifanya kazi na jeshi la Marekani na raia wa Marekani walikwama nchini humo.

Licha ya wakosoaji kusema Rais Biden aliyatelekeza masharti ya kuyaondoa kwa ukamilifu majeshi ya Marekani nchini Afghanistan lakini katika mahojiano na barua yake ya kujizulu ambayo Shirika la Habari la AP imeapata nakala yake Khalilzad anasema walijadili masharti ya namna ya kuondoka kwa majeshi hayo na Taliban pamoja na kuingia katika mazungumzo kabambe na serikali ya Afghanistan.

Chanzo: AP