1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa Marekani yuko Doha kuzungumza na Taliban

10 Agosti 2021

Mwakilishi maalum wa Marekani katika mazungumzo ya maridhiano ya Afghanistan, Zalmay Khalilzad, atalishinikiza kundi la Taliban kusitisha operesheni yake ya kijeshi katika mazungumzo ya Doha wiki hii

Afghanistan Zalmay Khalilzad in Kabul
Picha: AFP/W. Kohsar

Mwakilishi maalum wa Marekani katika mazungumzo ya maridhiano ya Afghanistan, Zalmay Khalilzad, atalishinikiza kundi la Taliban kusitisha operesheni yake ya kijeshi katika mazungumzo ya Doha wiki hii, baada ya wanamgambo hao wa itikadi kali kukamata miji mikuu ya mikoa kadhaa. Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imesema balozi Khalilzad atakuwa Doha kusaidia kutayarisha jibu la pamoja la jamii ya kimataifa kwa hali inayoendelea kuzorota kwa kasi nchini Afghanistan

Soma pia:Taliban wauteka mkoa mwingine tena Afghanistan

Mazungumzo ya amani ya Afghanistan mjini DohaPicha: picture-alliance/AP Photo/Qatar Ministry of Foreign Affairs

Marekani imesema kasi iliyoongezeka ya mashambulizi ya Taliban, na kusababisha vifo na majeruhi kwa raia kazika vita hivyo kati ya pande mbili, na tuhuma za vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu mambo yanayozusha wasiwasi mkubwa.  Khalilzad amesema serikali ya Afghanistan na wanamgambo wa Taliban wako mbali zaidi kufikia makubaliano ya amani. Wataliban jana walikamata Aybak ambao ni mji mkuu wa jimbo la Samangan na wanasema wanasonga mbele kuingia katika mji wa Mazar-i-Sharif -- ambao ndio mji mkubwa kabisa kaskazini mwa nchi na kiungo muhimu kwa udhibiti wa serikali katika kanda hiyo.

Soma pia: Taliban wateka mji mkuu wa pili wa jimbo Afghanistan

Vikosi vinavyoiunga mkono serikali viliuacha mji huo wa Aybak na kukimbilia kwenye kilima cha Koh-e Bast baada ya serikali kuu kushindwa kupeleka nyongeza ya askari na haikutekeleza mashambulizi ya angani kuvisaidia vikosi vya serikali.

Hata hivyo mbunge mwingine kutoka kwenye eneo bunge hilo amesema askari wengine wapya 300 watapelekwa ili kusaidia operesheni ya kuwashinikiza Taliban kuondoka kutoka kwne mji wa Aybak, wenye wakazi zaidi ya 120,000.

Soma pia: Kundi la Taliban laudhibiti mji mkuu wa kwanza Afghanistan

Siku ya Jumapili wanamgambo wa Taliban waliiteka miji mikuu mitatu ya Kunduz, Sar-e Pul na Taluqan. Wapiganaji wa Taliban wamechukua zaidi ya nusu ya wilaya za Afghanistan wakati ambapo majeshi ya Marekani na NATO yanakamilisha hatua za kuondoka kabisa nchini humo.

AFP/DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW