Mjumbe wa Umoja wa Mataifa apewa saa 72 kuondoka Niger
11 Oktoba 2023Katika taarifa iliyosainiwa Oktoba 10, wizara ya mambo ya nje ya Niger imeamuru mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni raia wa Canada Louise Aubin kuondoka ndani ya saa 72. Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa mjini Niamey hajaeleza chochote.
Utawala huo wa kijeshi umeushutumu Umoja wa Mataifa kuwa walitumia kile walichokiita "ujanja usiofaa" uliochochewa na Ufaransa ili kuzuia ushiriki wake kamili katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa na mikutano mingine iliyofuata ya mashirika ya Umoja huo ambayo ilifanyika katika miji ya Vienna na Riyadh.
Maafisa wa jeshi walionyakua mamlaka katika mapinduzi mwezi Julai nchini Niger, hawakuwa na mwakilishi katika mkutano wa viongozi wa dunia huko New York.
Chuki ya mataifa ya Sahel dhidi ya Umoja wa Mataifa
Watawala wa kijeshi wa Niger wanafuata nyayo za nchi jirani ya Mali na Burkina Faso, ambazo pia zimedhihirisha chuki dhidi ya Umoja wa Mataifa na mkoloni wao wa zamani Ufaransa baada ya wanajeshi kutwaa pia madaraka. Niger tayari imechukua uamuzi wa kuwatimua wanajeshi na Balozi wa Ufaransa.
Burkina Faso ilimfukuza mratibu wa Umoja wa Mataifa mwaka jana huku Mali ikisitisha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ambao ulikuwa ukihudumu nchini humo kwa muongo mmoja.
Katika taarifa iliyotolewa leo hii, serikali ya Mali imefutilia mbali idhini iliyotolewa kwa shirika la ndege la Ufaransa "Air France" ya kuanza tena safari za ndege kuelekea nchini humo.
Nchi zote tatu zinapambana na uasi wa makundi ya itikadi kali za kiislamu ambao umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, na kupelekea maafisa wa jeshi kunyakua madaraka kwa ahadi ya kuimarisha hali jumla ya usalama.
Mapinduzi hayo yameambatana na shutuma za kwamba Ufaransa imekuwa na ushawishi mkubwa katika makoloni yake ya zamani, jambo lililosababisha tawala za mataifa hayo ya Sahel kuielekea Urusi na kuichukulia kama mshirika wa kimkakati badala ya Ufaransa ambayo hata hivyo imekuwa ikikanusha kutumia ushawishi usiofaa katika mataifa hayo.
Hayo yakijiri, leo hii msafara wa kwanza wa wanajeshi wa Ufaransa umeanza kuondoka mjini Niamey huku Marekani ikitangaza kusitisha msaada wa dola milioni 500 kwa Niger na kutoa wito wa kurejesha haraka iwezekanavyo utawala wa kidemokrasia.
Marekani ambayo bado ina jumla ya wanajeshi wapatao 1,000 nchini Niger, imesema kwa sasa wanajeshi wake hawatoi tena mafunzo au kuvisaidia vikosi vya Niger lakini wataendelea na shughuli za kufuatilia kwa karibu vitisho kutoka kwa makundi ya kigaidi.
(Chanzo:AFP)