1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa UN aonya kuhusu kuzuka vita kamili Myanmar

11 Agosti 2021

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar Christine Schraner Burgener ameonya kuhusu kuzuka kwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa pande zote nchini humo hazitafanya mazungumzo

Myanmar Training der Opposition
Picha: AFP

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar Christine Schraner Burgener ameonya kuhusu kuzuka kwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa jeshi lenye nguvu, wafuasi wa serikali ya kidemokrasia iliyoangushwa, makundi ya kikabila na pande nyingine muhimu hawatafanya mazungumzo ya kufana kuhusu masuala yote kuanzia mlipuko wa sasa wa COVID-19 hadi mizizi ya mgogoro wa nchi hiyo. 

Soma zaidi: Utawala kuwafutia mashtaka waandamanaji Myanmar

Schraner Burgener amewaambia waandishi wa habari kuwa makabiliano kati ya jeshi na vikosi vya ulinzi vya ndani yanaendelea, watu wana hofu na wanateseka na hakuna uhuru wa kujieleza. "Tumeona vurugu nyingi nchini humo. Watu wengi wanahofia kiwango kikubwa cha vurugu za kijeshi, lakini pia Vikosi vya Ulinzi wa Wananchi vinatumia sasa silaha zaidi na zaidi ambazo sio za kujitengenezea lakini pia ni silaha za kitaalamu zaidi. Hivyo, natumai kuwa mazungumzo yanawezekana ili kuepusha kuzuka kwa vita vya kamili vya wenyewe kwa wenyewe."

Christine Schraner Burgener aelezea wasiwasi MyanmarPicha: Anthony Anex/Keystone/picture alliance

Benki ya Dunia inatabiri kushuka kwa asilimia 18 katika Pato Jumla la Ndani mwaka huu na Shirika la Kazi la Kimataifa - ILO linakadiria kuwa nafasi za kazi milioni 2.2. zimepotea tangu Januari. Zaidi ya hayo, mjumbe huyo amesema Myanmar kwa sasa inakabiliwa na wimbi kali la tatu la COVID-19, huku kukiwa na zaidi ya visa 333,000 vilivyoripotiwa.

Soma pia: Umoja wa Mataifa waikosoa Myanmar kuhusu demokrasia

Schraner Burgener amesema kiongozi wa kijeshi, Jenerali Mkuu Min Aung Hlaing, anataka kuendeleza udhibiti wake madarakani, akitaja tangazo la karibuni la kumtaja kuwa waziri mkuu, kufutwa kwa uchaguzi wa Novemba na hofu kuwa chama cha kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung Suu Kyi cha NLD kitavunjwa hivi karibuni.

Soma pia:Myanmar yaanza kuwaachilia huru wafungwa wengine 2,300

Katika majadiliano yake mapana na pande zote nchini Myanmar amesema aligundua kuwa hakuna pande zozote zitakazolegeza msimamo na kuwa tayari kufikia makubaliano yoyote.

Kwa miezi miwili, Schraner Burgener amesema alijadili pendekezo lake na pande muhimu nchini Myanmar na Jamii ya kimataifa. Ambalo ni kuundwa Kundi la Kimataifa la Uangalizi linalozijumuisha China, Japan, India, Thailand, Marekani, Uingereza, Norway, Uswisi, Umoja wa UIaya, Umoja wa Mataifa na Jumuiya Mataifa ya Mashariki mwa Asia - ASEANambayo Myanmar ni mwanachama. Amesema makundi ya kikabila yenye silaha yanaunga mkono wazo.

Soma pia:Jeshi Myanmar lajiongezea miaka miwili madarakani

Mjumbe huyo amesema alifanya pia mazungumzo marefu na naibu mkuu wa jeshi Soe Win kuhusu masuala mengi likiwepo pendekezo la kuanzisha mazungumzo, lakini hakupewa jibu. Hata hivyo, anasema mazungumzo yataanza karibuni kupitia ASEAN na mjumbe wake mpya kwa Myanmar, waziri wa pili wa mambo ya kigeni wa Brunei Erywan Yusof.

AP