1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa UN kwa Myanmar azungumza na kiongozi wa kijeshi

18 Agosti 2022

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Mynamar, Noeleen Heyzer, amekutana na kiongozi wa utawala wa kijeshi wa taifa hilo na kumtolea wito wa kusitisha machafuko na kufungua milango ya kurejea utawala wa kiraia.

Myanmar UN Noeleen Heyzer  Min Aung Hlaing
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar, Noeleen Heyzer alipokutana na kiongozi wa kijeshi wa Myanmar, Jenerali Min Aung HlaingPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Mwanadiplomasia huyo wa Umoja wa Mataifa, Noeleen Heyzer, aliyekuwa nchini Myanmar kwa ziara ya siku mbili amekutana na Jenerali Min Aung Hlaing, anayeongoza Baraza Tawala la kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka uliopita na kujadiliana naye bila kificho ajenda zinazoitia tumbojoto Jumuiya ya Kimataifa linapohusika suala la Mynamar.

Bibi Heyzer alisafiri hadi mji mkuu wa Myanmar, Naypyitaw, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa nchi hiyo inayoandamwa na mzozo.

Taarifa iliyotolewa na ofisi yake imesema, kwanza alimweleza Jenerali Min wasiwasi mkubwa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya kuzorota kwa hali ya kiutu, usalama, uchumi na siasa nchini Mynamar tangu jeshi lilipotwaa madaraka.

Wakati wa mazungumzo hayo mjumbe huyo maalumu alimrai Jenerali Min kukomesha machafuko nchini Myanmar, kufungua majadiliano ya kuirejesha nchi hiyo katika mkondo wa kidemokrasia na kushughulikia suala la kiongozi wa kiaraia aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi.

Heyzer "aliuma jongoo kwa meno" alipokutana na Jenerali Min

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar, Noeleen Heyzer alikutana pia na waziri wa mambo ya kigeni wa Myanmar, Wunna Maung LwinPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Suala la kuachiwa wafungwa wa kisiasa na dhima ya serikali ya Mynarmar kwenye ukandamizaji wa jamii ya wachache ya waislamu wa Rohingya nayo yalikuwa sehemu ya ajenda za majadiliano.

Kadhalika aliliweka mezani suala la adhabu ya kifo nchini Myanmar ambapo amemuhimiza Jenerali Min kuweka zuio kwa hukumu za watu kunyongwa. Wito huo unafuatia kuyongwa hivi karibuni kwa wanaharakati wanne wa kisiasa, tukio lililosababisha ukosoaji mkubwa wa kimataifa.

Taarifa ya ofisi ya mjumbe huyo maalum inasema bibi Heyzer hakuyapaka mafuta matamshi yake wakati wa mazungumzo na Jenerali Min, alimweleza bayana mambo yote na hapa ninanukuu sehemu ya alichokisema

``Umma wa Myanmar una haki ya demokrasia na uwezo wa kujiamulia hatma yake bila woga na shinikizo na hilo litawezekana kwa dhamira na juhudi za wadau wote chini ya mchakato shirikishi" mwisho wa kunukuu.

Mpango wa kusonga mbele na hatma ya Suu Kyi vyachagiza mazungumzo 

Kiongozi wa kiraia aliyeondolewa madaraka nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi Picha: Koen van Weel/picture alliance /ANP

Ili kusonga mbele kwenye masuala yaliyozungumzwa, taarifa kutoka ofisi ya mwanadiplomasia huyo imesema, yeye na kiongozi wa kijeshi wa Mynamar wamekubaliana kuendelea kufanya mazungumzo kwa uwazi na kutafuta majibu kuelekea Myanmar yenye amani na ya kidemokrasia.

Mjumbe huyo aliwasilisha mpango unaofafanua njia za Myanmar kurejea katika mkondo unaokubalika kimataifa.

Sehemu ya mapendekezo ni pamoja na jeshi kuchukua hatua za kutuliza mzozo na kuzileta mezani pande zote nchini humo kutafuta jawabu la kisiasa litakaloiwezesha nchi hiyo kutawaliwa tena na raia.

Ama kuhusu suala la kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi, bibi Heyzer amependekeza kwa watawala wa kijeshi wamwachie huru na kumruhusu kutoka gerezani anakotumikia vifungo vya muda tofauti.

Hata hivyo wakati wa ziara hiyo, bibi Heyzer hakufanikiwa kukutana na Suu Kyi ambaye bado anakabiliwa na mkururo wa kesi ambazo chama chake kinasema zimechochewa kisiasa.

Mynamar imetumbukia kwenye mzozo mkubwa tangu jeshi lilipochukua madaraka Februari mwaka jana. Jumuiya ya Kimataifa na asasi za kikanda ikiwemo kundi la mataifa ya ASEAN zimekuwa zinatafuta namna ya kuumaliza mapigano na makabiliano ambayo baadhi ya watu wanayafananisha na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW