1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa UN Syria ataka vikwazo viondolewe baada ya Assad

15 Desemba 2024

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria, Geir Pedersen, ametoa wito wa kuondolewa haraka vikwazo vya mataifa ya Magharibi dhidi ya taifa hilo kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Bashar Assad.

Kordan|  Mjumbe maalum wa UN Syria Geir Pedersen
Geir Pedersen, kulia, mjumbe maalumu wa UN kuhusu Syria amefanya ziara mjini Damascus, Jumapili Desemba 15, 2024, na kupendekeza vikwazo vya mataifa ya magharibi dhidi ya taifa hilo viondolewe baada ya kuangushwa kwa utawala wa Bashar al-Assad.Picha: Andrew Caballero-Reynolds/Pool via REUTERS

Serikali ya Syria imekuwa chini ya vikwazo vikali vya Marekani, Umoja wa Ulaya, na mataifa mengine kwa miaka mingi kutokana na ukandamizaji wa Assad dhidi ya maandamano ya amani yaliyotokea mwaka 2011, ambayo baadaye yaligeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya karibu nusu milioni ya watu na kuwahamisha nusu ya wakazi wa milioni 23 wa Syria kabla ya vita.

Ujenzi mpya umezuiliwa kwa kiwango kikubwa na vikwazo ambavyo vililenga kuzuia ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa na mali katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali bila suluhu ya kisiasa.

Geir Pedersen, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, amesema wakati wa ziara yake mjini Damascus kuwa ni muhimu kuona vikwazo vikiondolewa haraka ili kuruhusu juhudi za kujenga upya Syria.

Alisisitiza kuwa suluhisho la kudumu kwa Syria linapaswa kujumuisha wananchi wote na kuongozwa na Wasyria wenyewe.

"Tunatumai kuona mwisho wa haraka wa vikwazo ili tuweze kuona uhamasishaji wa karibu wa ujenzi wa Syria," Pedersen aliwaambia waandishi wa habari wakati wa ziara ya Damascus.

Pedersen alizuru Damascus kukutana na maafisa wa serikali ya mpito iliyoundwa na wapinzani wa Assad, ikiongozwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS).

Assad akimbia nchi, waasi waukamata Damascus

01:45

This browser does not support the video element.

HTS imeorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto kwenye juhudi za ujenzi wa upya. Hata hivyo, maafisa wa Washington wamesema utawala wa Biden unazingatia kuiondoa HTS kutoka orodha ya makundi ya kigaidi.

Soma pia:Waziri Mkuu mpya wa mpito wa Syria Mohammad al-Bashir aahidi kuwatendea haki raia wote Syria

Serikali hiyo ya mpito itatawala hadi Machi, lakini bado haijatoa mwelekeo wa wazi kuhusu mchakato wa kuunda serikali mpya ya kudumu. Pedersen ameongeza kuwa ni muhimu kufanikisha mchakato wa kisiasa unaowashirikisha wananchi wote wa Syria.

Alitoa wito wa haki na uwajibikaji kwa uhalifu uliotendeka wakati wa vita, akisisitiza kuwa msaada wa kibinadamu unahitajika kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. Pedersen amehimiza hatua za haraka za kimataifa kusaidia kurejesha hali ya kawaida nchini Syria.

Amesisitiza kuwa kuondolewa kwa vikwazo kutakuwa hatua muhimu katika kuharakisha juhudi za ujenzi mpya na kuimarisha umoja wa taifa hilo baada ya miaka mingi ya mgogoro wa kisiasa na kibinadamu.

Wasyria zaidi ya 76,000 warejea nyumbani baada ya Assad kuanguka

Zaidi ya wahamiaji 7,600 wa Syria walivuka mpaka wa Uturuki kurejea nyumbani katika muda wa siku tano baada ya kuanguka kwa mtawala wa Syria, Bashar al-Assad, waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki alisema Jumapili.

Katika taarifa kwenye X, waziri wa mambo ya ndani, Ali Yerlikaya, aliorodhesha idadi ya wahamiaji wa Syria "waliorudi kwa hiari kutoka Uturuki" kila siku kati ya Desemba 9 na 13, ambapo jumla ya siku tano ilifikia wahamiaji 7,621. 

Uturuki inahifadhi karibu watu milioni tatu waliokimbia Syria baada ya kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011, huku kuanguka kwa Assad kukiamsha matumaini kwamba wengi watarejea nyumbani.

Mapema Jumatatu, waandishi wa AFP waliona mamia ya wakimbizi wakikusanyika katika kivuko cha mpakani cha Cilvegozu, takriban kilomita 50 magharibi mwa Aleppo, jiji la pili kwa ukubwa Syria, huku takwimu za wizara ya mambo ya ndani zikionyesha kuwa watu 1,259 walivuka siku hiyo. 

Watu wengine 1,669 walivuka Jumanne, 1,293 Jumatano, 1,553 Alhamisi, na 1,847 Ijumaa, Yerlikaya alisema. Ndani ya saa 48 baada ya kuanguka kwa Assad, Uturuki iliongeza uwezo wake wa kuvusha watu mpakani kila siku kutoka 3,000 hadi kati ya 15,000 na 20,000, Yerlikaya alisema mapema wiki hii. 

Wahamiaji wa Syria wakisubiri kwenye mpaka wa Cilvegozu ili kuvuka kuingia Syria, baada ya waasi kutangaza kumuondoa Rais Bashar al-Assad, katika mji wa Reyhanli, mkoani Hatay, Uturuki, Desemba 10, 2024.Picha: Dilara Senkaya/REUTERS

Uturuki inashiriki mpaka wa kilomita 900 na Syria ikiwa na vivuko vitano vinavoyfanya kazi, na imesema itafungua kivuko cha sita magharibi kabisa ili "kupunguza msongamano." 

Huku hisia za kupinga wakimbizi wa Syria zikiwa juu ndani ya jamii ya Uturuki, Ankara inataka kuona wakimbizi wengi kadri iwezekanavyo wakirejea nyumbani. 

Soma pia: Mohammed al-Bashir kiongozi wa mpito Syria

Karibu watu milioni 1.24 -- sawa na asilimia 42 -- wanatoka katika mkoa wa Aleppo, wizara ya mambo ya ndani imesema. 

Wanafunzi wengi warejea shuleni Damascus

Watoto waliovaa sare walionekana wakirudi shuleni mjini Damascus, siku ya Jumapili, wakihudhuria masomo kwa mara ya kwanza tangu kuanguka kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad wiki moja iliyopita. 

Shamrashamra katika mji mkuu wa Syria kufuatia kuchukuliwa kwa mamlaka na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) mnamo Desemba 8 sasa zimetoa nafasi kwa utulivu wa maisha ya kila siku. 

"Shule imetuomba kuwarudisha wanafunzi wa shule za kati na juu darasani," alisema Raghida Ghosn, mwenye umri wa miaka 56, mama wa watoto watatu.  "Wadogo wataanza kurudi shuleni baada ya siku mbili," aliiambia AFP.

Mfanyakazi wa shule moja alisema kuwa "si zaidi ya asilimia 30" ya wanafunzi walikuwa wamerudi darasani siku ya Jumapili, lakini "idadi hii itapanda polepole." 

Wanafunzi wakiwa wamekusanyika shuleni katika majira ya asubuhi kufuatia tangazo la mamlaka mpya kuhusu kufunguliwa tena kwa shule, baada y akumpindua mtawala wa Syria Bashar al-Assad, Desemba 15, 2024.Picha: Ammar Awad/REUTERS

Vyuo vikuu pia vilifunguliwa tena, lakini ni wafanyakazi wachache wa usimamizi walioonekana kazini Jumapili. "Wanafunzi wengi wanatoka mikoa mingine, kwa hivyo itachukua muda kwa mambo kurudi katika hali ya kawaida," alisema mfanyakazi mmoja wa chuo kikuu aliyekataa kutajwa jina. 

Shughuli za kibiashara pia zimerudi, huku watu wengi wakielekea kazini kama kawaida mapema Jumapili, siku ya kwanza ya wiki ya kazi nchini Syria. 

Soma pia:Waasi wa Syria waendelea kusonga mbele 

Mwandishi wa AFP aliona takriban watu kadhaa wakipanga foleni nje ya duka la mkate katika wilaya ya Rokn-Eddine mjini humo. Wauzaji wa barabarani waliokuwa wakinadi makopo ya petroli pia walionekana wakiendelea na biashara zao. 

Mjini Damascus, kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchi, umeme bado hukatwa mara kwa mara, huku baadhi ya maeneo yakikumbwa na ukosefu wa umeme wa hadi saa 20 kwa siku. 

Uturuki iko tayari kutoa msaada wa kijeshi kwa serikali mpya ya Syria: waziri wa ulinzi

Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yasar Guler, amesema Uturuki iko tayari kutoa msaada wa kijeshi kwa serikali mpya ya Syria, iwapo watahitaji msaada huo. Akizungumza Jumapili, Guler alisisitiza kwamba uongozi mpya unapaswa kupewa nafasi, na Uturuki iko tayari kutoa msaada muhimu ikiwa itahitajika.

"Ni muhimu kuona hatua zitakazochukuliwa na uongozi mpya," alisema Guler akizungumzia muungano wa waasi wa Hayat Tahrir al-Sham (HTS), ambao umetokana na tawi la Al-Qaeda nchini Syria na ulioorodheshwa kama shirika la kigaidi na serikali nyingi za Magharibi.

Hata hivyo, HTS imejaribu kupunguza mivutano kupitia kauli zake na serikali ya mpito imeahidi kulinda haki za Wasyria wote pamoja na kuheshimu utawala wa sheria. 

Uturuki yaishambulia Syria

01:01

This browser does not support the video element.

Guler alisema Uturuki ina mikataba ya mafunzo na ushirikiano wa kijeshi na nchi nyingi, na iko tayari kutoa msaada muhimu iwapo serikali mpya itauhitaji.

Alibainisha kuwa utawala mpya umeahidi "kuheshimu taasisi zote za serikali, Umoja wa Mataifa, na mashirika mengine ya kimataifa" na kutoa taarifa za ushahidi wowote wa silaha za kemikali kwa shirika la OPCW. 

Kipaumbele kikuu cha Uturuki nchini Syria ni kuondoa wapiganaji wa Kikurdi wanaotaka kujitenga, lengo ambalo liliungwa mkono na serikali mpya, Guler alisema.

Soma pia: Waasi wa Syria waingia Damascus, wasema Assad amekimbia

"Katika kipindi hiki kipya, shirika la kigaidi la PKK/YPG litaondolewa nchini Syria, mapema au baadaye. Sisi na serikali mpya ya Syria tunataka hili," alisisitiza. Pia aliongeza kuwa Uturuki haina matatizo na ndugu wa Kikurdi wanaoishi Iraq na Syria, bali tatizo ni kwa magaidi pekee. 

Hata hivyo, msimamo wa Uturuki kuhusu YPG na PKK unakinzana vikali na msimamo wa Marekani, mshirika muhimu wa vikosi vya SDF vilivyoongoza mapambano dhidi ya kundi la Dola ka Kiilslamu (IS) mwaka 2019.

Uturuki inaiona YPG kama tawi la PKK, adui wa ndani aliyepigana na serikali ya Uturuki kwa miongo kadhaa. Guler alihitimisha kwa kusema, "kipaumbele chetu nchini Syria ni kukomesha shirika la kigaidi la PKK/YPG," na alieleza kuwa Uturuki inatarajia Marekani kutathmini upya msimamo wake. 

Chanzo: mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW