Mkakati wa Ujerumani kuhusu China wavutia hisia tofauti
14 Julai 2023Waraka wa mkakati wa serikali ya Ujerumani kuhusu China, uliyozinduliwa hivi karibuni umepata maoni tofauti huko Asia ya Kusini-Mashariki, huku China ikiupuuza kuwa "haufai" lakini Taiwan ikiukaribisha kama hatua ya kusonga mbele.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, wakati huohuo, alitaka siku ya Ijumaa kuzihakikishia kampuni zinazofanya biashara nchini China kwamba utawala wake hautaki kudhibiti vitega uchumi nchini China licha ya lengo pana la kupunguza utegemezi wa kiuchumi wa Ujerumani kwenye uchumi wa China ambao ni wa pili kwa ukubwa duniani.
Soma pia: Ujerumani yazindua mkakati mpya wa kuamiliana na China
Mkakati wa kwanza kabisa wa serikali ya Ujerumani kuelekea China, waraka wa kurasa 61 unaoelezea mtazamo na mkakati wa serikali kwa China, ulitolewa Alhamisi baada ya miezi kadhaa ya mjadala wa ndani.
Unatoa wito wa "kusawazisha" uhusiano wa Berlin na Beijing, ambao umeundwa na mizozo inayoongezeka ya kimaeneo na ushindani wa biashara katika miaka ya hivi karibuni.
Katika waraka huo, serikali ya Ujerumani pia inaishutumu Beijing kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na juhudi za kudhoofisha sheria za kimataifa na siasa zake za nguvu za uchokozi katika eneo la Indo-Pasifiki.
China: Mkakati utazidisha mgawanyiko duniani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin alisema Ijumaa mjini Beijing kwamba waraka huo "utazidisha tu mgawanyiko wa dunia."
Pia ameishutumu serikali ya Ujerumani kwa ulinzi wa kiuchumi kuhusiana na mkakati huo, unaotaka makampuni ya Ujerumani kupunguza utegemezi wa kupindukia kwa wasambazaji au watumiaji wa China.
Wang alisema China ilikuwa na matumaini kwamba Ujerumani itachukuwa "mtazamo mpana na usioegemea upande" wa maendeleo ya nchini China.
Soma pia: Scholz azungumza na China kutumia ushawishi wake kwa Urusi
Wadadisi wa kisiasa nchini Taiwan, wakati huo wameufasiri mkakati wa Ujerumani kuelekea China kama ishara kwamba suala la kujitegemea kwa taifa hilo limezidi kuhamia zaidi katikati mwa nadhari ya kimataifa.
"Kukiri kwamba kuongezeka kwa mzozo wa kijeshi katika Mlango-Bahari wa Taiwan kungeathiri maslahi ya Ujerumani na Ulaya ni uthibitisho kwamba amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan ni suala la kimataifa," alisema Hung Mao-nan, profesa wa chuo kikuu cha Tamkang mjini New Taipei.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Taiwan alisema Ijumaa mjini Taipei kwamba Taiwan itafanya kila iwezalo "kufanya kazi na Ujerumani na washirika wengine wenye nia kama hiyo kuendelea kujenga utaratibu wa usalama wa kimataifa unaozingatia sheria, kuimarisha mifumo ya ugavi ya kidemokrasia na kuimarisha uthabiti wa kidemokrasia duniani. "
Ingawa mkakati wa Ujerumani kuhusu China ulisisitiza "Sera ya China Moja", ambayo inakataa kuitambua Taiwan kama nchi huru, unaionya China dhidi ya kujaribu kuchukua tena kisiwa hicho kwa nguvu.
Soma pia: Ujerumani, China zafanya mazungumzo ya ngazi ya juu
"Mabadiliko ya hali iliyopo katika Mlango-Bahari wa Taiwan yanaweza tu kufanyika kwa amani na kwa makubaliano ya pande zote," ulisema waraka huo.
Scholz awapa matumaini wafanyabiashara
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alipuuza athari za mara moja za mkakati huo kwa biashara za Ujerumani wakati wa mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, akisema kuwa serikali haina nia wala uwezo wa kufuatilia kwa karibu shughuli za kila siku za biashara.
Scholz pia alisema kuwa makampuni mengi ya Ujerumani tayari yanahamisha uwekezaji wao na kudhibiti hatari zinazohusiana na soko la China kulingana na kile mkakati unachopendekeza.
"Maoni yangu ni kwamba makampuni mengi yataendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa nchini China, yatauza nje ya China na pia yatanunua bidhaa na huduma kutoka China," Scholz alisema.
Soma pia: China yasema Beijing inapendelea ushirikiano na Ujerumani
Lakini anatarajia makampuni "wakati huo huo, kwa maana ya kile tunachoita kupunguza hatari, kutumia fursa zinazotokea kwao kufanya uwekezaji wa moja kwa moja mahali pengine, ikiwa ni pamoja na kwa mfano mahali pengine barani Asia."
Wakati huo huo, Scholz alisisitiza kwamba serikali ya Ujerumani inapanga kufanya uangalizi zaidi juu ya maeneo nyeti: "Yumkini ni wazi kwamba tunataka kuangalia kwa karibu masuala ambayo ni muhimu kwa usalama wa kijeshi na usalama kwa ujumla."
Chanzo: DPAE