Mkanganyiko kuhusu muswada wa huduma za habari Tanzania
10 Februari 2023Tamko hilo limejiri siku moja baada ya Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa kusema kuwa muswada huo hauwezi kusomwa katika kikao cha sasa bungeni.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amelazimika kuitisha kikao cha dharura na wanahabari baada ya kuwepo kwa utata kuhusu uwasilishwaji wa muswada wa sheria ya huduma za habari, uliotakiwa kuwasilishwa bungeni Ijumaa.
Alhamisi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alitoa taarifa kwamba muswada huo hautaweza kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Bunge unaokwisha Jumamosi, badala yake utasomwa katika mkutano ujao wa Bunge.
Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote wakwama Tanzania
Wakati huo huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema muswada wa mabadiliko ya sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 utatua bungeni Ijumaa Februari 10, 2022.
Novemba 21 mwaka jana Waziri Nape alipokea mapendekezo ya wadau wa habari ambayo walitaka mabadiliko katika Sheria ya Huduma za habari ambayo inatajwa kuwa kandamizi na kutaka kubadili baadhi ya vipengele ikiwamo mamlaka makubwa aliyonayo Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya kufungia gazeti.
Mchakato wa kudai mabadiliko hayo uliongozwa na Wajumbe wa Umoja wa Haki za Kupata Habari Tanzania, (Cori) ambao wanaitaka serikali kubadili vifungu vya sheria vilivyotaka chombo cha habari kuomba leseni kila mwaka, mabadiliko ya tafsiri ya neno uchochezi na udhalilishaji kuwa makosa ya jinai na kuondoa mamlaka ya mkurugenzi wa habari kukifungia chombo cha habari.
Florence Majani, DW, Dar es Salaam.