Mkanganyiko na hasira Guinea-Bissau baada ya mapinduzi
29 Januari 2026
Tangu uchaguzi wa mwaka 2025 na mapinduzi ya kijeshi yaliyofuata, Guinea-Bissau imekuwa katika hali ya msukosuko wa kisiasa, huku hali ya kutoaminiana na hasira ikitawala miongoni mwa vyama vya upinzani nchini humo.
Waziri wa zamani wa sheria, Carmelita Pires, aliiambia DW kuwa: "Kuna ushahidi wa wazi kwamba Rais aliyeondolewa madarakani, Umaro Sissoco Embalo mwenyewe, ndiye aliye nyuma ya kile kinachoitwa mapinduzi haya.”
Kwa mujibu wa Pires, dalili zinaonyesha kuwa mgombea wa upinzani, Fernando Dias da Costa, alishinda uchaguzi wa urais kwa ushindi mkubwa — matokeo ambayo Embalo, ambaye pia alikuwa mgombea, hakuyakubali. Anasema kuzuia kutangazwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi kuligeuka kuwa kipaumbele.
Mnamo Novemba 26, 2025, kundi la majenerali lilitwaa madaraka, siku moja tu kabla ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Serikali ya kijeshi, iliyoongozwa na Jenerali Horta Inta-A Na Man, ilidai ilichukua madaraka ili kulilinda taifa dhidi ya magenge ya dawa za kulevya na madai ya ushawishi wao katika siasa.
"Haya mapinduzi yalikuwa na lengo moja tu: kuandaa kurejea kwa Sissoco Embalo madarakani,” alisema Pires, ambaye tangu mapinduzi hayo anaishi nchini Ureno. Aliongeza kuwa viongozi wote wa mapinduzi wanatoka katika mduara wa karibu wa rais huyo wa zamani.
Tangu wakati huo, Embalo hajatokea hadharani. Mara tu baada ya mapinduzi, alisafiri na wasaidizi wake kwenda Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo. Baada ya siku chache, aliripotiwa kupata hifadhi nchini Morocco. Hadi sasa, mahali alipo haswa bado hapajulikani.
Taifa lililo katika hali ya sintofahamu
Uchaguzi wa wabunge uliofanyika siku hiyo hiyo ya uchaguzi wa urais pia ulitangazwa kuwa batili. Uchaguzi huo tayari ulikuwa na utata kwa sababu chama kikubwa cha upinzani, PAIGC (Chama cha Afrika cha Uhuru wa Guinea na Cape Verde), kilizuiwa kushiriki kwa misingi ya kisheria.
Tangu hapo, Guinea-Bissau imebaki bila taasisi za serikali zinazofanya kazi. Mamlaka pekee iliyopo ni ya kijeshi, ambayo, kwa mujibu wa Carmelita Pires, inaendesha nchi "kama bwana wa kifalme.”
Katika wiki za hivi karibuni, shughuli zote za kisiasa zimepigwa marufuku, ikiwemo maandamano na migomo. Ofisi za vyama zimefungwa, Mahakama ya Katiba imesimamishwa, na mikutano na waandishi wa habari imekatazwa bila kibali cha awali. Wanaharakati wengi wa asasi za kiraia na wanasiasa wamekamatwa.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Domingos Simões Pereira, kiongozi wa chama cha PAIGC, ambaye amekuwa akizuiliwa kwa zaidi ya siku 60 katika kituo cha polisi mjini Bissau. Kwa binti yake, Denisa Pereira, hali hiyo haikubaliki.
"Kila mtu anajua kuwa mazingira ambayo baba yangu anashikiliwa ni ya kinyama,” aliiambia DW.
Denisa Pereira pia aliikosoa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), akiishutumu kwa kutochukua hatua.
"Najiuliza ECOWAS bado ina jukumu gani. Wawakilishi wake walipata fursa ya kujionea hali ya baba yangu lakini walichagua kutomtembelea. Ni nini kingine kinapaswa kutokea?”
Wito wa uingiliaji wa kijeshi
Katika maandamano dhidi ya mapinduzi ya kikatiba ya Novemba 26, Mariano Quade, mmoja wa viongozi wa juu wa kampeni ya urais ya Fernando Dias da Costa, alitoa wito kwa ECOWAS kuingilia kijeshi ili kurejesha utawala wa kidemokrasia.
Alionya kuwa kushindwa kuchukua hatua kutasababisha jumuiya hiyo kupoteza uaminifu wake kabisa.
"Uingiliaji wa kijeshi ndio chaguo pekee lililobaki kwa ECOWAS,” Quade alisema akiwa Lisbon katika mahojiano na shirika la habari la Ureno, Lusa.
"Katika hali ya mapinduzi ya kijeshi na sera ya kutovumilia tawala za mapinduzi, ECOWAS ina njia moja tu: kutumia nguvu kurejesha mamlaka kwa wananchi,” aliongeza.
Uchaguzi Desemba?
Shinikizo la kimataifa dhidi ya utawala wa kijeshi mjini Bissau linaongezeka. Guinea-Bissau imesimamishwa uanachama na Umoja wa Afrika, ECOWAS, na Jumuiya ya Nchi zinazozungumza Kireno (CPLP).
Kwa kujibu, uongozi wa kijeshi ulionekana kupunguza makali, ukitangaza mwezi Januari kwamba uchaguzi ungefanyika Desemba 6 na kwamba utaratibu wa kikatiba ungerudishwa.
Hata hivyo, kufanya uchaguzi mwaka huu kunaonekana kuwa jambo gumu. Rais wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE), N'pabi Cabi, alimweleza rais wa mpito Horta Inta-A kwamba tume hiyo haina uwezo wa kuandaa uchaguzi bila vifaa vipya. Mbali na uhaba wa fedha, alisema hata masanduku ya kupigia kura hayapo.
"Katika mji wa mbali wa Bafata, kwa mfano, hakuna hata sanduku moja la kupigia kura. Pia tunakabiliwa na matatizo makubwa ya mifumo ya kompyuta na hatuna hata kompyuta moja,” Cabi alisema baada ya mkutano na rais wa mpito katika mashauriano kuhusu ratiba ya uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi pia imependekeza kufanyika kwa usajili upya kamili wa wapiga kura kabla ya uchaguzi ujao.