1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yasema haitaki

Mtullya Abdu4 Mei 2016

Mustakabali wa mazungumzo juu ya kufikia mkataba wa kuanzisha biashara huru baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya, TTIP umezidi kuingia mashakani. Ufaransa imetishia kuupinga mkataba huo

Rais wa Ufaransa Francois Hollande
Rais wa Ufaransa Francois HollandePicha: Reuters/S. de Sakutin

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema nchi yake asilani haitakubali wakulima na utamaduni wake ukabiliwe, na changamoto kwa sababu tu ya kuwezeshwa kuingia katika masoko ya Marekani. Rais Hollande amesema kwa sasa Ufaransa inasema haitaki.

Waziri asisitiza msimamo

Hapo awali Waziri wa biashara Matthias Fekl aliiambia Europa 1 Radio kwamba, mazungumzo juu ya kufikia mkataba wa kuanzisha biashara huru baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya yamekwama na kwamba kuyasimamisha kunaweza kuwa njia bora.

Waziri huyo, amesisitiza juu ya ulinzi wa mazingira na maslahi ya wakulima wa Ufaransa. Bwana Fekl amesema Ulaya inatoa mengi, lakini inapewa kigodo kutoka upande mwingine.

Mazungumzo juu ya mkataba wa biashara huru yameingia katika utata baada ya walinzi wa mazingira-Greenpeace, kufichua hati zinazobainisha njama zinazofanywa na Marekani. Kwa mujibu wa walinzi hao wa mazingira, Marekani inakusudia kuingiza katika mkataba bidhaa za kilimo zilizobadilishwa uasilia wake.

Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya biashara ya Umoja wa Ulaya Ignacio Garcia Bercero, ameeleza kwamba hati iliyofichuliwa inalionyesha pendekezo la Marekani juu ya kile wanachoita bidhaa za kilimo za tekinolojia ya kisasa, lakini kimsingi ni bidhaa za kilimo zilizobabilishwa vinasaba "GMOs".

Ishara ya mkataba wa kuleta biashara huru baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya ,TTIPPicha: picture-alliance/dpa/A. Bugi

Amesema mtu anaweza kubainisha kwamba hakuna pendekezo kutoka upande wa Umoja wa Ulaya. Mkurungenzi huyo ameeleza kuwa, kifungu hicho kinachohusu bidhaa za kilimo kimewekwa ndani ya parandesi ( mabano.)

Na mkuu wa kitengo cha siasa kwenye shirika la walinzi wa mazingira Stefan Krug amelalamika kwamba, watu karibu Bilioni moja watakaoathirika na matokeo ya mazungumzo nchini Marekani na barani Ulaya hawapewi habari juu ya mazungumzo hayo.

Hata hivyo Marekani imesema haina wasi wasi mkubwa, juu ya kufichuliwa kwa hati zinazojadiliwa kwenye mazungumzo ya kufikia mkataba wa kuanzisha biashara huru baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Mwandishi wa Ikulu, Josh Earnest, amesema Rais Obama ameeleza wazi juu ya mkakati wa Marekani kuhusu biashara ya kimataifa.

Mwandishi huyo wa Ikulu amesisitiza kwamba, Marekani inakusudia kuyakamilisha mazungumzo na Umoja wa Ulaya kabla ya Rais Obama kuondoka madarakani.

Lakini upinzani dhidi ya mkataba wa TTIP, unazidi kuongezeka barani Ulaya kutokana na tofauti za vigezo vinavyotumika katika kulinda maslahi ya wananchi.

Mwandishi:Mtullya Abdu.afp, dpa,

Mhariri:Yusuf Saumu