1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa DP World wageuka ajenda ya kisiasa Tanzania

Deo Kaji Makomba
31 Julai 2023

Suala la mkataba wa bandari kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai limegeuka mdahalo wa kisiasa, huku viongozi wa upinzani na chama tawala wakishindana kutumia mikutano ya hadhara kuumbuana.

Symbolbild CPTPP
Picha: Bayne Stanley/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Hatua ya chama tawala (CCM) kuzunguka katika maeneo mbalimbali kuunadi mkataba wa bandari uliozua mjadala nchini humo, inafuatia upinzani uliojitokeza kutoka kwa vyama vya siasa, wanasheria na makundi mbalimbali ya wanaharakati wanaoupinga mkataba huo baina ya Tanzania na kampuni DP World ya Dubai kwa hoja kuwa "umeuza bandari ambayo ni urithi wa Tanzania."

Akizungumza katika moja mikutano yake ya hadhara katika mji mkuu wa kiuchumi wa Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo, alisema chama chake, ambacho ndio kimeshika dola, "kinatekeleza ilani yake ikiwemo kuwaletea wananchi maendeleo".

Soma zaidi: Vuta n'kuvute vyama vya siasa Tanzania kuhusu DP World

Katibu Mkuu huyo alitumia lugha ya vijembe akiwataka wananchi kutowasikiliza wapinzani ambao "hawana hoja bali ni vioja."

CHADEMA yachanja mbuga na DP World

Wakati chama tawala kikizunguka kuwaeleza wananchi kile kinachosema ni mazuri ya mkataba huo, chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) kimeendelea na mikutano yake ya hadhara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kikiukemea na kuupinga kwa kudai kuwa "ni mkataba ulioiuza rasilimali muhimu ya vizazi vya Tanzania."

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.Picha: Eric Boniphace/DW

Akiwa kwenye mkutano wa hadhara mkoani Kagera, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Tanzania Bara, Tundu Lissu, alisema "biashara ya bandari ni roho ya nchi".

Tangu kuzuka kwa kadhia ya mkataba huo, kuimeibuka pande mbili zikipingana.

Soma zaidi: Waziri Makame Mbarawa atetea makubaliano na DP World

Upande mmoja unawakusanya wanasiasa wa upinzani kutoka CHADEMA, wanasheria, viongozi wa makanisa na wanaharakati wanaoelemea upande wa upinzani.

Upande mwengine wapo viongozi wa CCM na serikali pamoja na baadhi ya viongozi wa dini wanaouelezea kuwa ni mkataba wenye manufaa.

Imetayarishwa na Deo Kaji Makomba/DW Dodoma