Mkataba wa Gaza na hatma ya amani na matumaini
14 Oktoba 2025
"Karibuni nyumbani", huo ndio ulikuwa ujumbe uliochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Israel ikiwakaribisha nyumbani mateka waliochukuliwa na kundi la Hamas miaka miwili iliyopita.
Mikanda ya video iliyotolewa na jeshi la Israel ilionesha nyakati zilizojaa hisia nzito pale familia zilipowaona tena watoto, ndugu na jamaa zao baada ya miezi 24.
Ulikuwa wasaa wa kuungana tena na wengi hawakuamini kama alivyoelezea mjomba wa Eitan Horn, mmoja wa mateka walioachiwa huru mapema wiki hii.
"Miaka miwili ya jinamizi. Nimepitia mengi mazito maishani mwangu, na nilimudu kuyavuka, lakini miaka hii miwili iliyopita, ilikuwa migumu mno, nilihisi siwezi tena kustahamili. Ni jambo jema sana kwamba tumefikia hatua hii, kwamba ninaweza tena kutabasamu na kushusha pumzi."
Kurejea nyumbani kwa mateka 20 waliokuwa hai wa Israel ni sehemu ya mpango ulioandaliwa na Rais Donald Trump wa Marekani.
Chini ya makubaliano hayo mbali ya mateka walio hai, kundi la Hamas litakabidhi miili ya mateka wengine 27 waliokufa au kuuawa wakiwa kiuzuini.
Makundi ya watu yalikusanyika mjini Tel Aviv kuwakaribisha nyumbani mateka wao walibubujikwa machozo ya furaha pale taarifa za kuachiwa kundi la kwanza zilipotolewa. Hata hivyo wale ambao ndugu na jamaa zao ni miongoni mwa waliopoteza maisha, huzuni yao haikujificha.
Furaha na mwanzo mpya Ukanda wa Gaza, je, vitadumu?
Kwenye ukanda wa Gaza makubaliano ya kusitisha vita yameleta ahueni, lakini eneo hilo la Wapalestina linakabiliwa hivi sasa na mzozo mkubwa wa kibinadamu baada ya sehemu kubwa kushambaratishwa kwa vita.
Na kwa hakika safari ya kuijenga upya Gaza itakuwa ndefu. Usitishaji vita umewezesha zaidi ya wafungwa na mahabusu 2,000 wa Kipalestina kuachiwa huru. Walipokewa kwa furaha sana walipoingia Gaza na Ramallah huko Ukingo wa Magharibi.
Mmoja ya wafungwa wa Kipalestina aliyeachiwa huru ni Zaid Al-Jundi ambaye amesema, "Hatimaye tumepata tena uhuru wetu. Tumetoka jela, kaburi la walio hai, huru kutoka minyonyoro ya vizuizi, tunajiunga tena na familia, marafiki na watoto. Shukrani kwa kila mmoja".
Hata hivyo, wachambuzi na wanadiplomasia wanatahadharisha kuwa furaha na matumaini vinaweza kusambaratisha iwapo vipengele muhimu vya mkataba wa kusitisha vita havitatekelezwa au ikashindikana kuviwekea mpango wa utekelezaji.
Mojawapo ni makubaliano ya kulipokonya silaha kundi la Hamas na kulisambaratisha ili lisiwe na jukumu lolote katika uongozi wa Gaza mnamo siku za usoni.
Mtaalamu wa Mashariki ya Kati katika Kituo cha Masuala ya Kimataifa cha Washington, Jon Alterman, anasema mkataba wenyewe hakueleza kwa ufasaha hilo litatekelezwa vipi na hilo linaweza kuacha mwanya wa mabishano mnamo siku zinazokuja.
Kwa tathmini yake, anasema hakuna mkataba wa kimataifa ulioacha mianya mingi kama uliofikiwa hivi majuzi kati ya Israel na kundi la Hamas.
Trump atamudu kuendeleza shinikizo kwa Netanyahu?
Suala jingine litakalokuwa kihunzi kirefu ni kifungu kinachagusia uwezekano wa kuundwa taifa la Palestina. Wachambuzi wanasema kwa Waisraeli wengi hilo litakuwa gumu kulikubali hasa baada ya shambulizi la Oktoba 7.
Balozi wa zamani wa Marekani nchini Israel, Dan Shapiro, anasema ikiwa viongozi wa serikali na wanasiasa wa Israel watapiga kampeni kubwa ya kukataa kuundwa taifa la Palestina, itakuwa vigumu kwa nchi za kiarabu kulishawishi kundi la Hamas kutimiza wajibu wake chini mkataba wa Trump.
Upo wasiwasi vilevile kuhusu ni kwa umbali gani rais Donald Trump ataendelea kujihusisha na mzozo wa Mashariki ya Kati na kuendeleza shinikizo kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Trump anafahamika kwa kukosa ustahamilivu pale mazungumzo ya kusaka mwafaka yanapochukua muda mrefu.
Rais wa taasisi inayotafiti sera za kigeni za Israel ya Mitvim, Nimrod Goren anasema mwaka ujao utakuwa wa uchaguzi mkuu nchini Israel, na mahesabu yote ya Netanyahu yatahama kutoka kumridhisha Trump na badala yake ataelekeza nguvu ya kupambania hatma yake ya kisiasa.
Hii itajumuisha kuitoikasirisha kambi yake ya kihafidhina na misimamo mikali na hilo linaweza kutibua karibu kila kitu kinachosifiwa sasa au kama alivyojinasibu Trump mwenyewe kuwa "mwanzo wa enzi mpya katika kanda ya Mashariki ya Kati"