1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia waidhinishwa

Zainab Aziz Mhariri: Tatu Karema
25 Oktoba 2020

 Nchi 50 zimeidhinisha mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupiga marufuku silaha za nyuklia. Makubaliano hayo yatawezesha kuanza kutekelezwa kwa mkataba huo katika muda wa siku 90.

IAEA-Flagge
Picha: AFP/J. Klamar

Wanaharakati wanaopinga matumizi ya nyuklia wameisifu hatua hiyo lakini Marekani na mataifa mengine yenye nguvu yanayomiliki nyuklia wameupinga vikali mkataba huo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezipongeza nchi hizo 50 na amesifu kazi muhimu iliyofanywa na asasi za kiraia katika kuandaa mazungumzo na kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema mkataba huo utakaoanza kutekelezwa Januari 22 mwakani ni kilele cha harakati za ulimwenguni kote za kuwakumbusha watu juu ya matokeo mabaya kwa binadamu kutokana na matumizi ya silaha za nyuklia na pia ni harakati za kuwakumbuka watu walioathiriwa na milipuko ya nyuklia ikiwa ni pamoja na athari za majaribio ya silaha hizo, ambapo wengi wao ni miongoni mwa walioutetea mkataba huu. Guterres amesema mkataba huu unawakilisha hatua ya kujitolea inayolenga kuondolewa kabisa silaha za nyuklia, jambo ambalo linapewa kipaumbele na Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: UNTV/AP/picture-alliance

Beatrice Fihn, mkurugenzi mtendaji wa kampeni ya kimataifa ya kutokomeza silaha za nyuklia, muungano ulioshinda tuzo ya amani ya nobel ya mwaka 2017 ambao juhudi zake zilisaidia kupatikana kwa mkataba huo, amesema hatua hii imechukua muda wa miaka 75 tangu kutokea mashambulio ya kutisha ya Hiroshima na Nagasaki kulikowezesha kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ambao uliweka kipaumbele suala la kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia.

Marekani imeyaandikia mataifa yaliotia saini mkataba huo na kusema serikali yake inaamini kuwa yalifanya ''kosa la kimkakati'' na imeyahimiza kubatilisha misimamo yao.

Kwa mujibu wa shirika la habari Associated Press, Marekani imeziandikia barua nchi zilizotia saini mkataba huo inayosema kuwa utawala wa rais Trump unaamini kuwa zimefanya kosa la kimkakati na imezihimiza kukiuka makubaliano hayo. Marekani inasema mkataba huo wa kupiga marufuku silaha za yyuklia, unaojulikana kama TPNW, unarudisha nyuma juhudi za upokonyaji wa silaha hizo na pia ni wa hatari.

Mkurugenzi mtendaji wa kampeni ya kimataifa ya kutokomeza silaha za nyuklia Beatrice Fihn amesisitiza kuwa mkataba uliofikiwa utatekeleza lengo la kuzuia kuenea silaha za nyuklia na hatimae kuondoa kabisa matumizi ya silaha za nyuklia duniani.

Vyanzo:/AP/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW