Mkataba wa ulinzi wa Pakistan na Saudi unamanisha nini?
22 Septemba 2025
Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif wa Pakistan, nchi pekee ya kiislamu iliyo na silaha za nyuklia duniani, ndio waliousaini mkataba huo katika sherehe iliyohudhuriwa pia na Mkuu wa Majeshi wa Pakistan, Asim Munir, mjini Riyadh, Jumatano iliyopita. Kwa mujibu wa matamko yaliyotolewa na wizara ya nje ya Pakistan na shirika rasmi la habari la Saudi Arabia, mkataba huo unasema wazi kwamba: "Uchokozi wowote dhidi ya nchi moja utachukuliwa kuwa uchokozi kwa zote mbili. Makubaliano haya yanakusudia kukuza uwezo kwenye ushirikiano wa ulinzi baina ya nchi hizi mbili na kuimarisha hatua ya pamoja dhidi ya uchokozi wowote."
Japokuwa ni machache sana yanayohusu mkataba huyo yaliyowekwa wazi hadi sasa, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Mohammad, alisema siku moja baada ya kutiwa saini kwamba programu ya nyuklia ya nchi yake itakuwa tayari kutumiwa na Saudi Arabia endapo itahitajika chini ya makubaliano hayo.
Akijibu swali kwenye kituo kimoja cha televisheni siku ya Alkhamis, waziri huyo wa ulinzi alisema na hapa namnukuu: "Wacha niweke wazi jambo moja kuhusiana na uwezo wa nyuklia wa Pakistan: Uwezo huo ulithibitika zamani sana tulipokuwa tunafanya majaribio. Tangu hapo, tuna vikosi vilivyofunzwa kupambana kwenye uwanja wa vita kwa kutumia uwezo huo. Tulichonacho chochote kitakuwa pia cha Saudi Arabia kwa mujibu wa makubaliano haya." Mwisho wa kumnukuu.
Saudia inataka kuonyesha ufakhari wa kuwa na ushirikiano na Pakistan
Ushirikiano wa mataifa haya mawili una mizizi ya kidini, maslahi ya kimkakati na utegemeano wa kiuchumi. Kwa upande mmoja, Pakistan ni taifa pekee lenye Waislamu wengi ambalo lina nguvu za kinyuklia na, kwa upande mwengine, Saudi Arabia ni taifa linalojichukulia kama kiongozi wa Waislamu duniani, lakini lenye maslahi yake ya kiuchumi kwa Pakistan. Na kwa pamoja, zote mbili, Pakistan na Saudi Arabia, ni washirika wakubwa wa Marekani kwenye maeneo yao.
Kwa sasa, kuna takribani wanajeshi 1500 mpaka 2,000 wa Pakistan ndani ya Saudi Arabia, ambao wanatoa msaada wa kiufundi na mafunzo kwa jeshi la Saudia. Nayo Saudi Arabia imetowa mabilioni ya dola kwa njia ya msaada kwa Pakistan, taifa linalokabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni.
Mtaalamu wa masuala ya ulinzi mwenye makaazi yake London, Uingereza, Ghaffar Hussain, ameiambia DW kwamba kwa Saudi Arabia mkataba huu ni suala la kuonesha ufakhari wa kuwa na ushirikiano na taifa lenye nguvu za kinyuklia na kwa Pakistan, unaipa heshima ya kuonekana kuwa na nafasi kwenye jukwaa la kikanda, mambo ambayo nchi zote mbili zimekuwa zikiyapigania.
Kwa upande mwengine, muda uliotiwa saini mkataba huu nao una nafasi yake: ilikuwa ni siku chache baada ya Israel kuishambulia Qatar, mshirika mkubwa wa Marekani, kwa madai ya kuwalenga viongozi wa Hamas. Mashambulizi hayo yalichukuliwa na washirika wa Marekani kwenye Ghuba ya Arabuni kuwa ni ishara kuwa hayako salama na wala hayawezi kulindwa na Pentagon, madhali tu mshambuliaji ni Israel, na kwamba lazima yawe na mshirika mbadala, ambaye katika mfano huu, amekuwa ni Pakistan.