1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine na Urusi zarefusha muda wa usafirishaji wa nafaka.

18 Mei 2023

Maafisa wa Ukraine na Urusi wamekubali kurefusha kwa miezi miwili muda wa makubaliano ya kusafirisha nafaka ambao uliokuwa karibu kumalizika. katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres ameipongeza hatua hiyo.

Ukraine I Weizen Export
Picha: Andrew Kravchenko/AP/picture alliance

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amefahamisha kwamba muda wa usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine kwenda kwenye soko la kimataifa umerefushwa kwa miezi miwili zaidi katika makubaliano mapya yaliyofikiwa kati ya Ukraine na Urusi.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.Picha: ANKA

Mpango huo unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa unaruhusu usafirishaji wa nafaka kupitia kwenye Bahari Nyeusi. Maafisa wa Ukraine na Urusi wamethibitisha makubaliano ya mpango huo unaoruhusu usafirishaji nje nafaka licha ya vita vinavyoendelea.

Naibu Waziri Mkuu wa Olexandr Kubrakov, ambaye pia ni waziri maendeleo ya miundombinu wa Ukraine amesema kutokana na makubaliano hayo mapya, nafaka zitaendelea kusafirishwa kwa kipindi cha miezi miwili zaidi angalau hadi Julai 18. Kurefushwa kwa mkataba huo pia kumethibitishwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Uturuki. Guterres amesema mkataba huo ni muhimu kwa ajili ya uhakika wa upatikanaji wa chakula duniani na kwamba bidhaa za Ukraine na Urusi zinahitajika pakubwa katika kuilisha dunia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.Picha: FEISAL OMAR/REUTERS

Kutokana na kurefushwa kwa mkataba huo kuumeruhusu tani zipatazo milioni 30.3 za nafaka kuondoka katika bandari za Ukraine. Hesabu hiyo inajumuisha takriban tani 625,000 za vyakula kwa ajili ya shughuli za misaada nchini Afghanistan, Ethiopia, Kenya, Somalia na Yemen.

Ukraine na Urusi zote ni wauzaji wakuu wa ngano, mafuta ya alizeti na bidhaa nyingine za chakula kwa mataifa ya Asia na Afrika. Nchi hizo mbili zilizo kwenye vita zilitia saini makubaliano kwa mara ya kwanza mwaka jana. Mpango huo unasimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki.

Ukraine na Urusi zote ni wauzaji wakuu wa nafaka katika mataifa ya Asia na Afrika.Picha: Ukrinform/dpa/picture alliance

Baada ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine mnamo mwezi Februari mwaka 2022, usafirishaji wa nafaka ulisimama na kusababisha kupanda kwa bei za vyakula mnamo mwaka jana hali iliyochangia mzozo wa chakula duniani.

Vyanzo:AFP/DPA