Mke wa Mursi ajitokeza hadharani
9 Agosti 2013Naglaa Mahmoud mke wa rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi amewaambia maelfu ya waungaji mkono mume wake jana(08.08.2013) waendelee na upinzani wao bila kujadi kitisho hicho kilichotolewa na viongozi wa serikali inayoungwa mkono na jeshi.
Naglaa Mahmoud alijitokeza kwa mara ya kwanza tangu jeshi kufanya mapinduzi hapo Julai 3, ambayo yalifuatia maandamano ya umma , wakitaka mume wake aondolewe kutoka madarakani.
Hapo kabla vyombo vya habari vya Misri vilieleza kuwa Naglaa alikuwa akishikiliwa pamoja na mume wake katika eneo ambalo halijulikani pamoja na watoto wake.
Apandishwa jukwaani
Waandamanaji katika eneo la Nasir mjini Cairo walishangiria alipowasili na kupanda jukwaani. Hakusema alikuwa wapi tangu yalipofanyika mapinduzi. Waandamanaji walisherehekea sikukuu ya Idd el fitr katika eneo hilo la Nasr, na mmoja kati ya waandamanaji alisema.
"Nimekuja hapa na kushiriki Idd pamoja na kundi hili ambalo limekuwa likikandamizwa, lakini nilitaka kuwapo kwangu hapa kuwe ni ujumbe kuwa tuko pamoja dhidi ya wale waliofanya mapinduzi."
Musri anashikiliwa pamoja na wasaidizi wake wa ngazi ya juu, idadi kubwa wakiwa wamehamishiwa katika jela hivi karibuni kusini mwa mji wa Cairo.
Wanakabiliwa na mashitaka ikiwa ni pamoja na kuchochea ghasia katika matukio mbali mbali ambayo yamesababisha ghasia kubwa zilizomwaga damu mitaani katika muda wa mwaka mmoja wa utawala wa Mursi.
Watoto wa Mursi
Watoto wa Mursi pia wamejiunga na maandamano hayo ya kundi la Udugu wa Kiislamu na wametoa wito wa kuachiliwa baba yao.
Viongozi wa mpito wa Misri pamoja na jeshi wamesema kuwa wataendelea na mpango wao wa haraka wa mpito ambao unatoa fursa ya uchaguzi ifikapo mapema mwaka ujao.Nae kkiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameonya leo kwamba mzozo wa kisiasa nchini Misri unaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Khamenei amesema kuwa matukio nchini Misri yanatia wasi wasi.
Wanadiplomasia kutoka mataifa ya kigeni pamoja na wizara za mambo ya kigeni za mataifa ya kiarabu wamejaribu kupatanisha na kufikia suluhisho la amani kati ya pande hizo mbili.
Hata hivyo ziara ya hivi karibuni ya seneta wa Marekani John McCain na Lindsey Graham ilizusha hasira wakati maseneta hao walipotoa wito wa kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa , wakiwa na maana viongozi wa udugu wa Kiislamu ambao wanatuhumiwa kwa kuchochea ghasia.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape
Mhariri : Abdul-Rahman, Mohammed