Hali ya wakimbizi wa ndani nchini Congo bado ni ya wasiwasi
5 Mei 2020Hali ya wakimbizi wa ndani nchini Congo bado ni ya wasiwasi kufuatia mapigano yanayoendelea baina ya jeshi na makundi ya wapiganaji na vile vile mashambulizi ya wapiganaji wa Maimai dhidi ya raia. Shirika linalowashughulikia wakimbizi la Norway linaelezea kwenye ripoti yake kwamba takriban watu milioni moja na laki saba walikimbia makaazi yao mwaka 2019. Idadi hiyo inaiweka Congo kuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya pili ulimwenguni baada ya Syria kwa idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.
Kwa jumla Congo ina wakimbizi wa ndani milioni 5, mkimbizi mmoja katika kila kumi ya wakimbizi wa ndani duniani anaishi nchini Congo, inaelezea ripoti iliyotolewa leo na shirika la wakimbizi la Norway.
Migogoro na mapigano vinaendelea kulazimisha maelfu ya raia wa Congo kuyahama makaazi yao katika majimbo ya Ituri, Kivu ya kusini na Kivu ya kaskazini ambako jeshi la nchi hiyo linayasaka makundi ya wapiganaji na vile vile kutokana na mashambulizi ya wapiganaji walioko huko.
Ripoti hiyo inaelezea kwamba mwezi Aprili pekee watu laki mbili waliyahama makaazi yao kwenye jimbo la Ituri. Mkuu wa shirika la wakimbizi la Norway nchini Congo, Maureen Philippon amesema kwamba ongezeko la machafuko huko wakati huu wa mripuko wa ugonjwa wa Covid-19 ni mchanganyiko wamajanga ambao unaweza sababisha machafuko. Maureen ameelezea kwamba raia wa Congo wana lazima ya amani wakati huu kuliko wakati mwengine wowote ili kupambana na ugonjwa wa virusi vya Corona.
Wakimbizi wahitaji misaada ya msingi
Umoja wa Mataifa unaelezwa kuwa watu wasiopungua milioni 16 nchini Congo wanahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu wa 2020. Shirika la Marekanai kwa ajili ya misaada USAID linaelezea kwamba asilimia 46 ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano nchini Congo wanakumbwa na utapiamlo.
Jean-Bosco Lalo, kiongozi wa asasi za kiraia jimboni Ituri amesema kwamba wimbi la wakimbizi wa ndani limeongezeka kwa mda wa miaka mitatu sasa kufuatia machafuko yanayoendelea kwenye maeneo kadhaa ya jimbo hilo.
''Leo idadi ya wakimbizi wa ndani ni zaidi ya milioni tatu.Na kuna watu ambao walikimbia mara kadhaa,kutoka kambi moja hadi nyingine.Idadi hiyo ya wakimbizi iliongezeka kufuatia mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la wapiganaji wa CODECO huko kwenye mtaa wa Mahagi.wakimbizi hawana masaada,watoto wamekufa na njaa''.
Shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa lilielezea kwamba machafuko yanayoendelea yanasababisha hata mashirika ya misaada kushindwa kufika katika maeneo kadhaa kutoa misaada ya msingi. Shirika hilo limesema mapigano yamesababisha nyumba nyingi kuteketezwa kwa moto. Kulingana na umoja wa mataifa, toka miaka miwili katika jimbo la Ituri na Kivu kaskazini inakadiriwa kuwa nyumba 88,000 zimeharibiwa kutokana na vurugu.