1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kujadili uzalishaji wa nishati ya upepo

24 Aprili 2023

Mataifa tisa ya Ulaya yanafanya mkutano wa kilele hii leo wenye lengo la kuongeza uzalishaji wa nishati ya upepo katika Bahari ya Kaskazini, uliochochewa na vita vya Ukraine na shinikizo la kuwepo na nishati jadidifu.

Belgien EU Gipfel Italien Frankreich Macron Meloni
Picha: Petr Kupec/CTK Photo/imago images

Mkutano huo ulioandaliwa na Ubelgiji katika mji wa pwani wa Ostend, unawaleta pamoja viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya ya Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Denmark, Uholanzi na Luxembourg na unahudhuriwa pia na rais wa halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen.

Norway na Uingereza pia zitashiriki mkutano huo, ingawa maafisa wa Ufaransa walisema waziri wa nishati wa Uingereza ataongoza ujumbe wa taifa lao na sio Waziri Mkuu Rishi Sunak ambaye hangeweza kuhudhuria.

Vipaumbele ni kuondokana na utegemezi wa nishati na ulinzi wa mazingira

Taarifa ya pamoja ya mataifa hayo iliyochapishwa katika jarida la kisiasa-Politico, imeweka msisitizo kuwa mataifa hayo yanahitaji mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo katika eneo la bahari, kwa kile ilichosema kufikia malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuondokana na utegemezi wa gesi ya Urusi na kuhakikisha usalama wa Ulaya na Uhuru wake.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya Roberta Metsola na Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Lengo la pamoja kwa mataifa hayo ni  kuongeza uzalishaji wa nishati ya upepo kutoka nguvu za gigawati 120 ifikapo 2030 kutoka gagawati 30 tu za sasa na pengine angalau 300 nguvu za gigawati ifikapo 2050. Mkutano huu wa kilele unaitwa wa Bahari ya Kaskazini ni wa pili kufanyika, baada ya awali mataifa manne miongomni mwa haya ya sasa katika mkutano wa mwanzo mwaka jana, ambayo ni Ubelgiji, Denmark, Ujerumani na Uholanzi kuamua ni muhimu kupanua wigo wa ushirikiano.

Utekelezaji wa upatikanaji wa nishati ya itokanayo na upepo utakuwa wa kasi

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo, alisema kwamba utazingatia "kasi ya utekelezaji", haswa kusanifisha vifaa vinavyohitajika kujenga miundombinu ya kuzalisha nishati ya upepo wa pwani haraka na kwa bei nafuu. Takriban maafisa waandamizi wa kampuni zipatazo 100 kutoka katika kampuni za usambazaji wa mitambo ya upepo wanashiriki katika mkutano huo.

Soma zaidi:Viongozi wa EU kujadili hali ya kiuchumi wa kikanda

Viongozi wanaoshiriki mkutano huo akiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, wamesisitiza haja ya kutafuta utaalamu na vifaa kama injini za upepo, betri na vinginevyo kutoka Ulaya badala ya kwingineko duniani. Katika kipindi hiki China inashikilia nafasi kubwa katika usambazaji wa vifaa vya nishati ya upepo.

Chanzo: AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW