Mkurugenzi mkuu wa IMF ameanza majukumu yake
1 Novemba 2007Staruss-Kahn mwenye umri wa miaka 58 amepata fursa ya kuliongoza shirika hilo muhimu la kimataifa la fedha kutokana na ahadi zake kwamba ataendeleza sera za mabadiliko katika shirika hilo na kubadili kabisa sera ambazo zimekuwa zinatumika toka kumalizika vita vya pili vya dunia.
Sera hizo zilizingatia tu nchi za Marekani na Ulaya kuendelea kudhibiti uongozi wa shirika la fedha duniani.
Bwana Kahn ambae anachukua uongozi wa shirika la fedha duniani IMF kutoka kwa Rodrigo Rato raia wa Uhispania anakabiliwa na masuala ya kisiasa ambayo yatahitaji kutatuliwa.
Masuala hayo yanahusu kufikiwa makubaliano juu ya kuzipa nguvu nchi wanachama zinazoinukia na ambazo zina uwakilishi mdogo katika shirika hilo miongoni mwa nchi wanachama 185 kufikia mwaka 2008.
Wachambuzi wanasema bwana Strauss-Kahn atakabiliwa na wakati mgumu kuzishawishi nchi za Ulaya hadi zitakapokubali kujipunguzia uwezo mkubwa wa kupiga kura.
Huku China na India zikiwa zinachangia pakubwa katika kukua uchumi wa dunia, hali ya wasiwasi inajitokeza katika nchi kama vile Marekani na nchi za Ulaya, nchi zinazoendelea nazo zinadai kwamba zinataka nafasi kubwa katika shirika hilo la kimataifa la IMF ambalo linasimia mustakabali wa fedha duniani.
Marekani ambayo inashikilia uwezo wake wa turufu ya Veto imesema kuwa haitotaka kujiongezea uwezo zaidi wa kupiga kura.
Ufaransa na Uingereza zina wasiwasi kuwa iwapo kutatokea mabadiliko katika mfumo wa kupiga kura ndani ya shirika la fedha la kimataifa basi huenda zikalazimika kusukumwa nyuma.
China ambayo uchumi wake unakua kwa haraka imefikia kuwa nchi ya nne duniani kati ya zile zinazoongoza kiuchumi nyuma ya Marekani, Japan na Ujerumani.
Mkuu wa taasisi ya sera za uchumi ya Oxford, Domenico Lombardi amesema ana imani kwamba mkurugenzi huyo mpya wa shirika la fedha duniani Strauss-Kahn na waziri wa fedha wa Italia Tommaso Padoa-Schioppa ambae amechaguliwa kuongoza kamati ya maelekezo ya IMF watafaulu kuzishawishi nchi za Ulaya zikubali mabadiliko.
Na njia moja ambayo inaweza kutumiwa na nchi za Ulaya ni kushirikiana pamoja na kuwa na kiti kimoja chenye nguvu katika shirika hilo la IMF.
Kwa sasa nchi za Ulaya zina nafasi nane katika bodi yenye viti 24.
Nchi zinazo inukia kama Brazil na Argentina zimeonya kuwa huenda nchi hizo zikajiondoa kwenye uanachama wa shirika la fedha duniani iwapo hakutatokea mabadiliko.
Utawala mpya katika shirika la kimataifa la fedha IMF umekuja sambamba na miito inayotolewa na nchi wanachama inayohimiza kuangaliwa kwa karibu mabadiliko ya mifumo ya fedha duniani na hali inayosababishwa na msukosuko katika soko la dunia, au pia kushuka kwa thamani ya dola na kupanda bei za mafuta pamoja na kutokuwa na urari katika uchumi wa dunia.
Wakati huo huo mkurugenzi mkuu mpya wa IMF Strauss-Kahn atahitajika kutafuta mbinu zingine za kuingiza mapato katika mfuko wa shirika hilo ambazo huenda ikalazimu kuuzwa kiwango fulani cha malimbikizo ya dhahabu ya shirika hilo