1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi nwa Viongozi Marekani ajiuzulu

24 Julai 2024

Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi wa Viongozi Marekani Kimberly Cheatle amejiuzulu, siku moja baada ya kukiri kuwa shirika hilo lilishindwa katika dhamira yake ya kuzuia jaribio la mauaji dhidi ya Donald Trump.

Mkuu wa Secret Service Kimberly Cheatle
Cheatle alikiri kuwa idara hiyo ilishindwa katika juhudi zake wakati wa mkutano wa kampeni wa TrumpPicha: Kevin Mohatt/REUTERS

Cheatle alikuwa chini ya miito ya pande zote za kisiasa ya kumtaka ajiuzulu baada ya mtu mmoja mwenye umri wa miaka 20 aliyekuwa na bunduki kumjeruhi rais huyo wa zamani Mrepublican na ambaye ni mgombea wa sasa wa uchaguzi wa rais. Kisa hicho kilitokea katika mkutano wa kampeni Julai 13 mjini Butler, jimbo la Pennsylvania.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Mrepublican Mike Johnson alisema uamuzi huo ulipaswa kufanywa wiki moja iliyopita akiongeza kuwa anafuraha kuwa Cheatle ameitikia wito wa Warepublican na Wademocrat.

Soma pia: Wakuu wa nchi walaani shambulio dhidi ya Trump

Rais Joe Biden alimshukuru Cheatle kwa huduma yake ya karibu miongo mitatu katika Idara ya Ulinzi wa Viongozi akisema alijitolea na kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya kulilinda taifa wakati wote wa taaluma yake. Waziri wa Usalama wa Ndani Alejandro Mayorkas amesema naibu mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi wa Viongozi Ronald Rowe, ambaye amekuwa katika shirika hilo kwa miaka 24, atahudumu kama kaimu mkurugenzi hadi mrithi wa Cheatle atakapotangazwa.