Mkurugenzi wa uchaguzi Tanzania asema anatishiwa
29 Septemba 2020Zikiwa zimebaki siku 29 hadi siku ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania, mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi nchini hapa Dk. Charles Mahera amesema kuwa pamoja na mafanikio ambayo tume anayoiongoza inajivunia, pia anapitia kipindi kigumu ikiwepo kupata vitisho kutoka ndani na nje ya nchi.
Soma pia: Kampeni zaendelea kupamba moto Tanzania
"Tumeshuhudia watu wa mataifa ya nje, hata mimi hapa nimeandikiwa barua na Mmarekani mmoja anajiita Amsterdam mwanasheria, akiitisha tume ya taifa ya uchaguzi. Kwa sababu watu wanalalamika huko nje kwamba wanaonewa, na kwamba yeye sasa huko nje ndio anajiona ana haki ya kuwajali watanzania kuliko sisi," alisema Dk. Mahera mbele ya waandishi habari katika ukummbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa wa Arusha.
"Kwa hiyo mjue kwamba kama taifa ni majaribu tuliyonayo watu muendelee kuyaombea. Unakuta mtu anasimama kwenye jukwaa, anasema fulani atakwenda the Hegue, sasa badala kutumia muda mwingi kueneza sera unaeneza vitisho.”
Soma pia: NEC yashughulikia pingamizi 100 kati ya 500
Maandalizi ya uchaguzi yaelekea kukamilika
Mbali na hayo tume ya taifa ya uchaguzi imebainisha kuwa maandalizi kuelekea siku ya kupiga kura oktoba 28 yamekamilika kwa asilimia 80 mpaka sasa huku akitoa onyo kali kwa wale wote wenye lengo la kuuza vitambulisho vyao vya kupigia kura, na kusema kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na wote watakaobainika wanatachukuliwa hatua kali za kisheri.
Akizungumzia suala la kampeni zinazoendelea, mkurugenzi huyo wa tume ya taifa ya uchaguzi amewataka wagombea kuendesha kampeni za kistaarabu na kufuata sheria.
Soma pia:Tume ya uchaguzi Tanzania yamuita Tundu Lissu
"Kumekuwepo na choko choko na makosa ya makusudi, kusudi mtu fulani afanyiwe fujo halafu alalamike kwamba ameonewa. Tumevumilia sana na IGP amevumilia sana lakini kuanzia sasa mtashangaa, watu watapigwa mabomu wakienda sehemu ambazo wameambiwa wasiende, na tumeona imeanza jana kule Nyamongo Tarime.”
Siku ya Jumatatu, chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema, kililalamika kurushiwa mabomu ya kutoa machozi na jeshi la polisi, wakati mgombea wa chama hicho alipopita kijiji cha Nyamongo kusalimia wakaazi wa eneo hilo akielekea kwenye kampeni.
Soma pia: Wagombea Tanzania walalamikia uhalifu kwenye kampeni
Walemavu watoa wito wa kuzingatiwa
Miongoni mwa wadau walioshiriki kikao hicho ni watu wenye makundi maalumu wakiwepo walemavu, ambao wametoa wito kwa tume kuandaa mazingira yatakayoyawezesha makundi yote wa watu kupiga kura.
" Wawekwe wakalimani kipindi hiki cha kampeni ili na sisi walemavu viziwi tuweze kuelewa wagombea wetu wanasema nini ili tuweze kuchagua viongozi bora,” alisema Ramadhani Abubakari, mlemavu wa kusikia ambaye maoni yake yalitafsiriwa na Agness Geofrey.
Soma pia:Tanzania yaihakikishia Marekani uchaguzi utakuwa huru
Tanzania bara na visiwani ina jumla ya majimbo 264 ya uchaguzi, huku idadi kubwa ya waliojiandikisha kupiga kura wakiwa ni vijana wa kati ya umri wa miaka 18 hadi 35.
Mwandishi: Veronica Natalis DW, Arusha.