Mkururo wa mashambulizi ya Urusi yawauwa watu 6 Ukraine
3 Novemba 2025
Kulingana na maafisa, mashambulizi hayo pia yamesababisha kukatika kwa nguvu za umeme kwa makumi kwa maelfu ya watu.
Watoto hao walikuwa wavulana wawili waliokuwa na umri wa miaka 11 na 14 kulingana na shirika la haki za kibinadamu la Ukraine.
Mashambulizi hayo ya Urusi yamesababisha kukatika kwa umeme katika eneo zima la Donetsk mashariki pamoja na karibu nyumba 58,000 katika eneo la Zaporizhzhia kusini.
Urusi yakanusha kuwalenga raia
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema mashambulizi hayo ambayo yaliwajeruhi dazeni ya watu, yanaonesha kuwa lengo la Moscow ni kuwadhuru raia na kutangaza kuwa taifa lake limeongeza ulinzi wake wa angani.
Urusi lakini inakanusha kuwalenga raia katika mashambulizi yake.
Urusi imekataa mwito wa Marekani wa kusitisha vita vyake nchini Ukraine vilivyodumu kwa karibu miaka 4 na badala yake kuendelea na operesheni yake ya ardhini na kuanza upya mashambulizi yake dhidi ya gridi ya umeme ya Ukraine.
Nchi zote mbili zimejipiga kifua kwa kupata ushindi katika mapigano ya mji muhimu wa mashariki wa Pokrovsk amako Ukraine inakabiliwa na shinikizo kutokana na mashambulizi ya Urusi yanayohusisha maelfu ya vikosi vya majeshi.
Mashambulizi hayo ya usiku kucha yanafanyika siku moja baada ya kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine Oleksandr Syrsky kutangaza alikuwa ametuma vikosi maalum katika mji wa mashariki wa Pokrovsk ambako Ukraine iko chini ya shinikizo.
Jawabu la Ukraine kwa mashambulizi ya Urusi
Mapema wiki iliyopita, Ukraine ilisema mamia ya wanajeshi wa Urusi waliingia katika mji huo na iwapo watauteka basi Urusi itakuwa imepigwa jeki katika propaganda yake.
Ukraine imejibu mashambulizi ya Urusi katika gridi yake ya umeme kwa kushambulia miundo mbinu ya mafuta na gesi ya Urusi.
Mamlaka nchini Urusi zinasema shambulizi la droni la Ukraine mapema Jumapili katika bandari ya Tupase katika Bahari Nyeusi liliteketeza lori la mafuta na kuharibu miundo mbinu ya bandari.
Picha kadhaa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha moto katika maeneo kadhaa ya bandari hiyo ingawa shirika la habari la AFP halikuweza kuzithibitisha picha hizo.