1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutamo wa viongozi wa Umoja wa ulaya Magazetini

Oumilkheir Hamidou
9 Machi 2017

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki na harakati za upelelezi za Marekani katika ubalozi wao mdogo mjini Franckfurt ni miongoni mwa mada magazetini

Brüssel EU-Gipfel Ankunft Angela Merkel, Deutschland
Picha: picture-alliance/dpa/Photoshot

Tunaanzia Brussels unakofanyika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya. Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten linasema mkutano huo unajadili mustakbal wa Ulaya. Tangu sasa ni dhahir kwamba mageuzi jumla ya Umoja wa Ulaya hayawezi kupatikana kwa haraka. Pupa hazina maana seuze tena katika mada kadhaa wanachama wake hawana msimamo mmoja. Ili kuleta mabadiliko jumla makubaliano ya Umoja wa Ulaya yatabidi yafanyiwe marekebisho. Na katika nchi nyingi za Umoja wa Ulaya wananchi wanabidi waulizwe maoni yao. Kutokana na maarifa yaliyopatikana kufuatia  kura za maoni nchini Uholanzi, Ufaransa na Danemark, hakuna yeyote mwenye kuunga mkono Umoja wa Ulaya atakaependelea zoezi kama hilo lifanyike. Afadhali kuendelea na mikataba ya umoja wa Ulaya kama ilivyo. Dhahir lakini ni kwamba Umoja wa Ulaya unabidi ujiimarishe. Mwongozo uliopendekezwa na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Jean-Claude Juncker ni wa maana; watu wasijishughulishe sana na mambo madogo madogo ya siasa za ndani za mataifa husika na badala yake Umoja wa ulaya ujishughulishe zaidi na masuala muhimu zaidi.

 

Mvutano kati ya Ujerumani na Uturuki wahanikiza magazetini

 

Magazeti takriban yote ya Ujerumani yameripoti kuhusu mazungumzo ya jana katika hoteli moja ya mjini Berlin kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel na mwenzake wa Uturuki Mevlüt Cavusoglu."Ingawa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki hazungumzii tena kuhusu "mtindo wa wanazi" lakini analalamika "kuna hisia za chuki dhidi ya dini ya kiislam" linaandika gazeti la "Der neue Tag". Hoja hizo zinatolewa na waziri wa serikali ambayo, inawakandamiza na kuwasumbuwa jamii ya wachache ya wakristo nchini humo linaendelea kuandika gazeti la der neue Tag, linalomaza kwa kusema uhuru wa kuabudu na uhuru wa mtu kutoa maoni yake watu wanaojivunia nchini Ujerumani, wakristo wanaoishi Uturuki wanauotea tu . Wakati umewadia kwa miko kama hiyo kuvunjwa.

Nalo gazeti la mjini Dresden "Sächsische Zeitung "linahisi hali itatulia baada ya kura ya maoni ya katiba kuitishwa mwezi unaokuja wa April nchini Uturuki. Kwasababu huo ndio mzizi wa fitina . Wapiga kura wa Uturuki wanaoishi Ujerumani ndio wanaolengwa. Kwa  mtazamo wa muda mrefu wanasiasa wa Ujerumani hawabidi kulinyamazia sawa na makubaliano ya wakimbizi pamoja na Ankara. Kwasababu mwenye kuridhia kila kitu ndie anaeonekana mwishoe kuwa mjinga linamaliza kuandika gazeti la "Sachsische Zeitung.

 

Wikileaks yafichua siri nyengine za upelelezi wa CIA Ujerumani

 

Gazeti la "Mannheimer Morgen" linazungumzia kuhusu ripoti ya mtandao wa kijamiii wa Wikileaks inayofichua harakati kubwa za upelelezi zinazofanywa na shirika la Marekani la CIA katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Frankfurt am Main. Gazeti linasema ripoti hiyo inaaminika kwasababu ilikuwa ikitarajiwa. Wataalam kwa miaka sasa wamekuwa wakitahadharisha dhidi ya udhaifu wa zana za elektroniki. Kwamba idara za upelelezi kazi yao kuitumia hali hiyo kukusanya habari, hilo si siri kwa yeyote yule. Yadhihirika kana kwamba idara za upelelezi hivi sasa hazikusanyi habari zao kupitia njia zile zile za zamani. Zinalenga zaidi  zana za elektroniki. Na mitandao inayozidi kuongezeka inawarahisishia mambo.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW