1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutanio wa G20 kwa maendeleo ya Afrika mjini Berlin

Oumilkheir Hamidou
13 Juni 2017

Mkutano wa siku mbili wa wa G 20 mjini Berlin kuhimiza vitega uchumi kwaajili ya bara la Afrika , lengo hasa ni nini? Na umuhimu wa Ujerumani na Ufaransa katika kuimarisha Umoja wa ulaya ni miongoni mwa mada magazetini

Deutschland G20 Afrika Treffen
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

 

Tunaanzia Berlin unakoendelea mkutano wa siku mbili  wa mataifa yanayoinukia kiuchumi na yale yaliyoendelea-G-20. Wahariri wanahisi lengo halisi ni kuzuwia wimbi la wakimbizi. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Sababu halisi ya kuvutiwa na bara la Afrika inakutikana kwengine kabisa: Inahusiana na namna ya kuzuwia mikururo ya wahamiaji. Waafrika wasije huku, bora wapatiwe kazi makwao na kusalia huko huko-hivyo ndivyo nchi za kaskazini zifikirivyo. Hikma hiyo haiwezi kukosolewa lakini inatatanisha. Ukuaji wa kiuchumi hauzuwii uhamiaji-kinyume kabisa. Katika miaka ya hivi karibuni ya neema vijana wengi  zaidi wa kiafrika walikimbilia Ulaya kuliko wakati wowote ule mwengine. Ghana, Senegal, Nigeria-si sadfa, kwamba wanaokuja ulaya wanatokea katika nchi zinazojimudu. Wasiojimudu hawana pesa wala nguvu za kuhama. Kwa hivyo panahitajika mengi zaidi ya ukuaji wa kiuchumi ili kuwatanabahisha watu wabakie makwao. Kwa kutanguliza mbele vitega uchumi vya kibinafsi kama injini ya maendeleo barani Afrika, nchi za G-20, hazijachangia bado katika kuung'owa mzizi wa fitina: rushwa. Ili watu wawe na matumaini mema ya maisha, wanahitaji elimu , huduma za afya na taasisi za serikali za kuaminika."

Au pengine lengo ni soko?

 

Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linahisi kwa upande wake lengo halisi hapo ni soko. Gazeti linaendelea kuandika: "Hadi ifikapo mwaka 2050 idadi ya wakaazi wa Afrika wataongezeka mara dufu na kufikia watu bilioni 2.5. Wawekezaji wanapukuta mikono-wanawaangalia na kuwalinganisha na wateja bilioni mbili na nusu."

Ujerumani na Ufaransa kuwajibika upya kuelekea Umoja wa ulaya

Injini ya Ujerumani na Ufaransa katika kuuimarisha Umoja wa ulaya ni mada iliyochambuliwa na mhariri wa gazeti la "Rhein-Zeitung" anaeandika: "Lengo kwa Ujerumani na Ufaransa linabidi liwe" kugeuka upya injini ya kuujongeza mbele Umoja wa Ulaya. Kwasababu madola hayo mawili makubwa kiuchumi barani Ulaya yanawajibika kuliunganisha ipasavyo bara la Ulaya, ili, mbali na China, Marekani na Urusi, liweze kuwa nguzo muhimu ya kiuchumi na kisiasa  ulimwenguni. Nchi za ulaya zitakapokuwa kitu kimoja tu ndipo zitakapoweza kujaza angalao kwa sehemu, pengo la hatari linalosababishwa na sera za mtengano za utawala mpya wa Marekani. Ulaya inahitaji sera ya kiuchumi inayotilia maanani zaidi ukuaji wa kiuchumi katika nchi za kusini mwa ulaya. Ujerumani haitakuwa na njia nyengine isipokuwa kuwekeza  zaidi na kwa masilahi yake mwenyewe, katika umoja wa Ulaya. Baada ya Brexit na baada ya kuchaguliwa Emmanuel Macron, Umoja wa Ulaya wa mataifa 27 una nafasi nzuri ya kujivumbua upya.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW