Mkutano juu ya masuala ya usalama waanza mjini Munich
15 Februari 2019Waziri wa mambo ya nje Maas amesema mkutano huo utakuwa fursa kwa Ujerumani kuonyesha jinsi ilivyojizatiti katika kuendeleza ushirikiano wa kimataifa. Waziri huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa kulinda uhuru wa kitaifa kutawezekana iwapo pana ushirikiano baina ya mataifa. Waziri Maas ameongeza kusema kuwa atafanya juhudi ili kuimarisha msimamo wa kuzingatia taratibu za kimataifa zinazoleta utulivu.
Wakati huo huo waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen amesema kabla ya kuanza mkutano huo wa mjini Munich ulio kusini mwa Ujerumani kwamba anakusudia kuepusha mgongano na Marekani juu ya suala la bajeti ya ulinzi ya nchi yake. Waziri von der Leyen aliliambia gazeti la Sueddeutsche kwamba Ujerumani tayari imeongeza matumizi katika jeshi lake kwa asilimia 36 katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Waziri Ursula von der Leyen ataufungua rasmi mkutano juu ya masuala ya usalama wa mjini Munich baadaye leo pamoja na mwenzake wa Uingereza, Gavin Williamson. Mambo yanayotarajiwa kutawala katika mkutano ni pamoja na hali ya mahusiano kati ya Ulaya na Marekani, kuongezeka kwa mivutano kati ya Urusi na nchi za Magharibi na migogoro ya Mashariki ya Kati.
Naibu waziri wa Ulinzi wa Marekani Pat Shanahan amewasili kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wa usalama mjini Munich unaoanza leo Ijumaa anatarajiwa kuwasilisha mkakati Marekani na washirika wake katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita dola la Kiislam IS.
Ujerumani imekuwa inabanwa na Marekani na nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO ikitakiwa iongeze mchango wake katika bajeti ya NATO kwa asilimia 2 ya pato lake jumla la taifa, kulingana na lengo lililokubaliwa na nchi wanachama wa NATO mnamo mwaka 2014.
Mwenyekiti wa mkutano huo juu ya usalama bwana Wolfgang Ischinger aliyewahi kuwa balozi wa Ujerumani nchini Uingereza na Marekani, amesema bara la Ulaya linapaswa kujiandaa kukabiliana na ushindani mkubwa katika biashara ya silaha na hasa inapohusu usalama wa nje na sera ya ulinzi. Ischinger amesema Ulaya kwa muda mrefu imekuwa ikijidanganya kwamba imezungukwa na marafiki na washirika jambo ambalo ni lazima sasa iurekebishe mtazamo wake.
Mapema mwezi huu, Marekani ilitangaza nia yake ya kujiondoa kutoka kwenye mkataba wa silaha za nyuklia kati yake na Urusi, kwa madai kwamba Urusi ilikiuka makubaliano ya mpango huo kwa kuendelea kutengeneza aina ya makombora ambayo hapo awali yalikuwa yamepigwa marufuku. Hatua hiyo imesababisha hofu na huenda ikaanzisha ushindani mpya wa kudhibiti silaha kati ya Marekani na Urusi.
Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE
Mhariri: Josephat Charo