1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu amani Libya waanza

12 Novemba 2018

Wahusika wakuu katika siasa za Libya wanakutana na viongozi wa dunia mjini Palermo nchini Italia kuanzia Jumatatu katika hatua ya nchi zenye nguvu duniani ya kuuanzisha upya mchakato wa kisiasa.

Giuseppe Conte
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Lami

Mchakato huo wa kisiasa uliokwama kwa muda mrefu huenda ukatoa nafasi kuwepo na uchaguzi. Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte anatarajia kamanda wa Libya Khalifa Haftar atahudhuria kuhudhuria mkutano huo wa siku mbili ili kuutilia mkazo mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuleta amani nchini Libya.

Maafisa wa Italia hapo Jumapili walikuwa wanafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba Haftar anahudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Italia. Iwapo atahudhuria huu utakuwa mkutano wake wa kwanza na Waziri Mkuu wa Libya aliye na makao mjini Tripoli Fayez al-Serraj tangu mkutano wa kilele mjini Paris ulioandaliwa mwezi Mei.

Hakuna uhasama baina ya Italia na Ufaransa kuhusu Libya

Katika mahojiano na gazeti moja la Italia, Conte amesema "nataraji Haftar atakuwepo kwa kuwa hakuna shaka kwamba yeye ni mmojawapo wa watu muhimu wanaohusika katika kuleta amani katika nchi yake," alisema Conte.

Kamanda wa Libya Khalifa HaftarPicha: Imago/S. Savostyanov

Waziri Mkuu Conte pia amepuuzilia mbali uhasama na Ufaransa kuhusu jinsi ya kuushughulikia mzozo wa Libya ambao umetokota katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta tangu kuondolewa madarakani kwa Muamar Gaddafi mwaka 2011.

Huku mkutano huo ukiwa unaanza Jumatatu, raia wa Libya mjini Tripoli ambao wanapitia wakati mgumu katika matumizi yao ya kila siku, wanasema hawana matumaini makubwa kwa kumalizika kwa mzozo wa kisiasa na kiuchumi nchini mwao. Imad Mohammed ni raia wa mjini Tripoli.

"Tunatarajia mazuri kutoka kwenye mkutano huo na suala lenyewe litatuliwe. Hali ya nchi inategemea maneno tu, makubaliano ya kumaliza matatizo," alisema Imad. "Haitegemei utumiaji wa silaha au tofauti za kidini au kikabila. Yote yanategemea makubaliano ya mchakato wa kisiasa. Ni mzozo wa kisiasa," aliongeza raia huyo wa Libya.

Hali imekuwa mbaya tangu kuondolewa madarakani Gaddafi

Mkutano wa kilele wa mwezi Mei mjini Paris ulishuhudia serikali ya Libya iliyoko Tripoli pamoja na kamanda Khalifa Haftar kukubaliana kufanya uchaguzi wa kitaifa Desemba 10 ila hilo halijafanyika.

Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-SarrajPicha: Imago

Umoja wa Mataifa umekiri kwamba tangu kuondolewa madarakani kwa Gaddafi hali haijawa shwari Libya na imesema uwezekano wa uchaguzi kufanyika nchini humo ni kuanzia mwakani katika kipindi cha machipuko.

Wachambuzi wanasema mkutano huo unaoanza leo uko katika hatari ya kuyumbishwa na taharuki iliyoko kati ya pande hasimu za Libya pamoja na ajenda zinazokinzana za nchi zenye nguvu.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef