1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu Mashariki ya Kati waanza Bahrain

Oumilkheir Hamidou
25 Juni 2019

Mkutano kuhusu maendeleo ya kiuchumi ya Wapalastina umeanza mjini Manama, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Marekani za kuufumbua mzozo kati ya Israel na Palestina. Lakini hakuna Mpalastina yeyote anaehudhuria mkutano huo.

Jared Kushner
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Walsh

Lengo la mkutano huo wa siku mbili ni kukusanya dala bilioni 50 kuwekeza katika kipindi cha miaka 10, lakini uamuzi wa viongozi wa Wapalastina kupinga kuhudhuria mkutano huo unawafanya watu washuku kama warsha hiyo iliopewa jina Amani kwaajili ya neema, italeta tija .

Serikali ya Israel haikualikwa.

Mkutano huo ni awamu ya kiuchumi ya kile kiitwacho "Makubaliano ya karne"-juhudi zilizokuwa zikisubiriwa kwa muda mrefu za ikulu ya Marekani kuhusu amani ya mashariki ya kati-na ambazo zinaongozwa na mkwe na mshauri wa rais Trump, Jared Kushner na mjumbe maalum Jason Greenblatt.

"Hatutohudhuria warsha hiyo"alisema kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina Mahmoud Abbas mwishoni mwa wiki."Sababu ni kwamba hali ya kiuchumi haipaswi kujadiliwa kabla ya hali ya kisiasa"ameongeza kusema.

Wapalastina wanataka masuala ya kina yajadiliwe kuanzia kanuni za mji wa Jerusalem na madai ya kuwa na taifa lao.

Mgomo jumla umeitishwa Gaza leo kulalamaika dhidi ya mkutano wa Bahrain. Maandamano yameitishwa pia katika maeneo ya ukingo wa magharibi wa mto Jordan. Taasisi za serikali na za kibinafsi, ikiwa ni pamoja na maduka na benki zimefungwa  ili kuwaruhusu watu washiriki katika maandamano.

Kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas asusia mkutano wa BahrainPicha: DW/T. Kraemer

Umoja wa Ulaya unawakilishwa kwa daraja ya kiufundi

Misri na Jordan nchi pekee za kiarabu zilizotiliana saini makubaliano ya amani pamoja na Israel zinasema zitawakilishwa na wasaidizi wa mawaziri wao wa fedha. Waziri wa fedha wa Saudi Arabia Mohammed al Jadaan ndie anaeongoza ujumbe wa nchi hiyo ya kifalme. Falme za nchi za kiarabu nazo pia zinawakilishwa. Umoja wa ulaya unawakilishwa kwa "daraja ya kiufundi."

Kwa mujkibu wa ikulu ya Marekani fedha zitakazopatikana zinabidi zitumike kubuni nafasi milioni moja za kazi kwaajili ya wapalastina na kugharamia shughuli za usafiri kati ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Mradi mwengine ni pamoja na kuimarisha miundo mbinu, shughuli za utalii na kilimo pamoja na kubuni miradi mengine nchini Misri, Lebanon na Jordan.

Serikali ya Donald Trump imevuruga sera ya miongo kadhaa ya Marekani kuelekea mzozo kati ya Israel na Palastina  kupitia maamuzi mfano kuhamishia ubalozi wa Marekani mjini Jerualem na kusitisha misaada.

Vyanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW