Mkutano kuhusu mzozo wa nyuklia wa Iran wafanyika mjini Vienna
22 Novemba 2007Hitilafu kubwa za maoni zinawatenganisha hasa wamarekani,Umoja wa Ulaya, na zile zinazojulikana kama makundi yasiyoelemea upande wowote. Mfarakano huo unaonyesha utaendelea kuwepo hata baada ya mkutano wa siku mbili wa shirika hilo unaoanza hii leo mjini Vienna.Wajumbe 35 wa baraza la magavana wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki wameanza mkutano wao wa mwishoni mwa mwaka hii leo mjini Vienna,mada kuu ikiwa mpango wa kinuklea unaozusha mabishano wa Iran.
Mkutano huo utakaodumu siku mbili utajishughulisha zaidi na ripoti ya kutatanisha ya mkurugenzi mkuu wa shirika la IAEA Mohammed Al Baradei kuhusu ushirikiano wa Iran pamoja na wataalam wa shirika hilo kwa lengo la kufafanua kwa undani kabisa malengo ya mpango wake wa kinuklea.
Wairan wanasisitiza mpango wao ni wa amani,lengo likiwa kutengeneza nishati,katika wakati ambapo Washington na baadshi ya nchi za magharibi zinaituhumu Iran kutaka kutengeneza silaha za kinuklea.
Akiufungua mkutano huo Mohammed El Baradei amesema shirika la IAEA halina uwezo wa kutoa hakikisho la dhati juu ya kutokuwepo vifaa na harakati za kinuklea ambazo hazikutajwa nchini Iran.
“Jambo hili ni muhimu zaidi hasa kwa upande wa Iran kutokana na historia yake kuhusu harakati zake ambazo hazikufafanuliwa na kutokana na haja ya kuwatanabahisha walimwengu kua mradi wa kinuklea wa Iran umelengwa kweli matumizi ya amani.” Amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki Mohammed El Baradei aliyeongeza,´Shirika la IAEA haina maelezo thabiti juu ya uwezekano wa kuwepo vifaa vya kinuklea ambavyo havikutajwa au harakati zozote za kutengeneza silaha za kinuklea nchini Iran.´´
Ripoti ya mkurugenzi mkuu wa shirika la nguvu za atomiki,Mohammed El Baradei, ambayo baadhi ya vifungu vilitangazwa tangu wiki iliyopita, inazungumzia kwa upande mmoja juu ya maendeleo yaliyopatikana katika kufafanua harakati za kinuklea za Iran na kwa upande wa pili ripoti hiyo inasema kwamba Teheran inaendelea kupuuza madai ya walimwengu ya kusitisha harakati za kurutubisha maadini ya Uranium,kama in na baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Hitilafu za maoni zimeanza tangu ripoti hiyo ilipojulikana.Kuna wanaofika hadi ya kusema Mohammed El Baradei anaitetea Iran anaposema,
“Mazungumzo ndio njia pekee ya kupatikana ufumbuzi wa mzozo wa Iran-na kila mazaungumzo yakianza haraka ndio bora kwa kila upande.´´
Hata kama magavana wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki hawatarajiwi kupitisha maazimio wakati wa mkutano wao,hata hivyo kikao hiki cha amwisho wa mwaka kinaangaliwa kama fursa kwa wanachama kuelezea maoni yao juu ya kadhia ambayo,baada ya ripoti ya Umoja wa ulaya kuhusu suala hilo hilo, inayotazamiwa kuchapishwa mwisho wa mwezi huu,inaweza kupelekea kutangazwa vikwazo vya Umoja wa mataifa dhidi ya Iran.