Mkutano kuhusu nishati ya nyuklia kuanza Ufaransa
10 Machi 2026
Mkutano wa kilele unaolenga kuongeza matumizi ya nishati ya nyuklia ya raia unafunguliwa mjini Paris leo Jumanne, huku mzozo wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ukionyesha hatari za kutegemea mafuta ya visukuku.
Wawakilishi kutoka takriban nchi 40 na mashirika ya kimataifa wanatarajiwa katika mkutano huo utakaofunguliwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. Marekani na China zitakuwepo, lakini Urusi, nchi nyingine muhimu ya nyuklia, haitakuwepo kwa sababu ya uvamizi wake nchini Ukraine.
Shirika la Nishati ya Atomiki la Umoja wa Mataifa (IAEA), ambalo ni mfadhili mwenza wa mkutano huo na Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), limesema kwamba uzalishaji wa nishati ya nyuklia unaweza kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050.
Linasema kwamba China inajenga vinu 29 ili kuongeza vinu vyake 57 ilivyonavyo ambavyo tayari vinafanya kazi.