Mkutano kutafuta suluhisho la mzozo wa Zimbabwe
26 Juni 2007Rais Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini mnamo mwezi wa Aprili,aliombwa na SADC kusaidia kusuluhisha mgogoro wa Zimbabwe.
Mkutano unafanywa nje ya mji mkuu wa Afrika ya Kusini,Pretoria.Mawaziri wa sheria na kazi wanaiwakilisha serikali ya Zimbabwe,wakati chama cha MDC kilichogawika kikiwakilishwa na wasemaji wake.
Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai ameweza kusafiri nje ya Zimbabwe kwa mara ya kwanza,tangu kupigwa kikatili pamoja na wengine darzeni kadhaa,hapo mwezi wa Machi walipojaribu kuhudhuria mkutano wa upinzani uliopigwa marufuku nchini Zimbabwe.
Rais Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini tangu miaka kadhaa anajaribu kusuluhisha mzozo wa kisiasa na kiuchumi wa Zimbabwe,lakini safari hii yadhihirika kuwa anaukabili kwa dhati zaidi, ujumbe aliokabidhiwa.
Kiini cha majadiliano hayo kati ya wajumbe wa ZANU-PF na MDC ni uchaguzi unaotazamiwa kufanywa mwezi Machi mwaka ujao na juhudi za Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kutaka kuibadilisha katiba. Mageuzi hayo pia yatampa Mugabe uwezo wa kubakia madarakani kwa maisha yake yote.
Kiongozi wa upinzani,Tsvangirai amesema,hataraji kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.Akieleza zaidi alisema hivi:
“Chaguzi kuu tatu zilizopita zilifanyiwa udanganyifu;sasa kipi kitakachomzuia kufanya udanganyifu mwingine tena.”
Katika majadiliano yanayofanywa,kuna masharti kadhaa yanayozingatiwa.Serikali ya Zimbabwe inasema,kabla ya cho chote,inataka upinzani utambue kuwa Rais Mugabe yupo madarakani kihaki. Hilo ni jambo lisilokubaliwa kabisa na upinzani, kwani ilidhihirika na kuthibitishwa na wasimamizi wa kimataifa na mashahidi kuwa kura zilifanyiwa hadaa,orodha ya wapiga kura ilikuwa na majina ya maelfu ya watu waliofariki na wapiga kura walitishwa vibaya na wafuasi wa serikali.
Hata hivyo,wataalamu wa siasa wanaamini kuwa hivi karibuni,lazima kutakuwepo mabadiliko nchini Zimbabwe.Kwani kiwango cha mfumuko wa bei ni kama asilimia 4500;idadi ya watu wasio na ajira ni asilimia 80;na Zimbabwe pia kwa sehemu kubwa, imetengwa na jumuiya ya kimataifa.
Kiongozi wa upinzani Tsvangirai amesema,wao wanashiriki katika majadiliano hayo kusaidia kampeni ya kuiokoa Zimbabwe na kuigutusha jumuiya ya kimataifa kutazama yale yanayotokea nchini humo.Amesema,wao wamedhamiria kuendelea kuipinga serikali,mpaka mageuzi ya kidemokrasia yatakapopatikana.
Matokeo ya mwanzo ya mazungumzo yanayofanywa sasa,yataelezwa na Rais Thabo Mbeki katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika utakaofanywa Ghana juma lijalo.