Mkutano kutathmini maendeleo yaliyopatikana Iraq
29 Mei 2008Katika mikutano iliyotangulia Iraq iliahidiwa msaada wa mabilioni lakini kilichotolewa ni kidogo.Miezi sita baada ya Irak kuvamiwa na Marekani,misaada iliyoahidiwa kutolewa kuijenga upya nchi hiyo,ilivutia mno.Kwa mfano mwaka 2003,katika mkutano wa kwanza kabisa ulioitishwa mjini Madrid, ilisemekana kuwa kutahitajiwa kiasi cha Dola bilioni 56.Marekani peke yake iliahidi kutoa bilioni 20.Misaada hiyo pamoja na mafuta ya Iraq yalitazamiwa kuleta maajabu ya kiuchumi nchini humo.
Mikutano mingine ikafuatliza nchini Jordan,Misri,Kuwait na sasa nchini Sweden.Kuna ahadi za misaada zaidi na kusamehewa madeni.Hata hivyo yadhihirika kuwa serikali ya Iraq imevunjika moyo baada ya kila mkutano,kama Waziri Mkuu Nouri al-Maliki alivyoeleza hivi karibuni mjini Kuwait.Alisema:
"Suala hapa ni nchi yetu kupatiwa msaada zaidi. Tunatumaini kuwa mkutano huu utakuwa na matokeo thabiti.Katika mikutano iliyopita,tuliunda kamati lakini hakuna kilichotekelezwa hadi hivi sasa."
Hasa nchi za Kiarabu ndio huadimika,linapozuka suala la msaada na ujenzi mpya wa Iraq.Kuwait inaendelea kudai fidia ya Dola bilioni 15 kugharimia hasara iliyosababishwa nchini humo baada ya kuvamiwa na Saddam Hussein mwaka 1990.Hata tajiri wa mafuta Saudi Arabia inadai Dola bilioni 17.Asilimia 75 ya madeni ya Iraq ni kutoka nchi sita za Ghuba.Isitoshe,Iraq inapaswa kulipa sehemu ya pato lake la mafuta katika mfuko wa Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo serikali ya Iraq inayodhibitiwa na Washia inasikitishwa kuona kuwa si Saudi Arabia wala Kuwait iliyokuwa tayari kufungua ubalozi mjini Baghdad sawa na nchi zingine za kiarabu zilizokuwa na Wasunni wengi.Sababu inayotolewa ni ukosefu wa usalama.Lakini sababu ni kuwepo kwa Marekani nchini Iraq na tuhuma kuwa Wasunni wanakandamizwa nchini humo.Lakini adui mkubwa wa zamani Iran ina uhusiano wa kibalozi na Iraq.
Mbali na ukosefu wa usalama,vile vile hakuna sheria kuhusu mafuta ya nchi hiyo-pato linaloweza kupindukia zaidi ya Dola bilioni 80 kwa mwaka.Makundi ya Kishia,Kisunni na Kikurd bado hayajakubaliana njia ya kugawana pato hilo.kwa hivyo,serikali haina budi isipokuwa kila mwaka kuahirisha kuwakaribisha wawekezaji wa mafuta huku wananchi wakiendelea kukosa takriban kila kita:umeme hupatikana kwa saa chache:maji ni nadra kupatikana na huduma za afya ni duni.Zaidi ya madaktari 2,000 wamefariki tangu kupinduliwa kwa Saddam Hussein na wengine 20,000 wamekimbilia nchi za kigeni.
Hadi hii leo,Iraq inangojea sehemu kubwa ya pesa zilizoahidiwa mjini Madrid miaka mitano iliyopita.Mwaka mmoja uliopita katika mkutano wa Sharm el-Sheikh nchini Misri,madola ya kimataifa yalitoa ahadi mpya za kusaidia mradi wa ujenzi mpya wa miaka mitano.Lakini ilhali hakuna usalama na ahadi za kupatikana maendeleo haziaminiki,basi umma utaendelea kuteseka.Safari hii mkutanoni Stockholm,Iraq haitazamiwi kupewa pesa zaidi bali waliotoa ahadi wataonywa kutimiza ahadi hizo na serikali ya Iraq nayo itahimizwa kuleta utulivu na upatanisho wa kitaifa.