Merz ataka Ujerumani isimame imara kimataifa
20 Februari 2026
Ujerumani inapaswa kusimama imara na kuchukuwa dhima kubwa zaidi katika jukwaa la dunia. Huo ni msimamo alioutowa Kansela Friedrich Merz kwenye mkutano mkuu wa chama chake cha CDU uliofunguliwa hivi leo mjini Stuttgart. Merz anatarajiwa kuwania tena nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho kwenye mkutano huo.
Mkutano mkuu wa chama cha Christian Democratic Union, CDU wa siku mbili unafanyika wakati ulimwengu ukishuhudia hali ya wasiwasi unaosababishwa na migogoro.
Kansela Friedrich Merz amewaambia wanachama wa chama chake kwamba utaratibu wa kidunia uliokuwa ukizingatia sheria za kimataifa haupo tena na kwahivyo Ujerumani inapaswa kusimama imara kujiweka mbele kimataifa na kuweka mikakati mipya katika Ulaya iliyo na mshikamano.
''Ulimwengu unapitia kipindi cha kujipanga upya. Ulaya inakabiliwa na shinikizo na Ujerumani inahitajika zaidi kuliko wakati mwengine wowote. Tunakabiliwa na changamoto kubwa. Tunataka kujiimarisha kiuchumi,tunataka kuilinda nchi yetu na kuifanya kuwa na nguvu zaidi za kijeshi. Tunataka kuendeleza ustawi endelevu wa taifa na tunahitaji kuimarisha sekta ya uvumbuzi kadhalika tunataka kuurudisha mshikamano wetu wa kijamii.''
Hotuba yake mjini Stuttgart kansela Merz imegusia masuala mbali mbali ya ndani ya nchi na ya kimataifa akikumbusha kwamba Marekani itabakia kuwa mshirika wa Ujerumani licha ya kuweko mivutano ya kisiasa na nchi hiyo.
Lakini katika siasa za ndani ameapa kutotowa mwanya kwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kuiharibu Ujerumani.
Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2021 alipondoka madarakani Kansela wa zamani Angela Merkel ameshiriki mkutano huo wa chama cha CDU akikaribishwa kwa makofi mengi na wanachama.Kansela Merz katika mtihani: jinsi anavyoshughulikia mgogoro wa serikali
Mara ya mwisho binafsi Merkel kushiriki mkutano huo ni mwaka 2019. Wamehudhuria pia viongozi wengine wa zamani wa chama hicho Annegret Kramp-Karrenbauer na Armin Laschet.
Pamoja na mengine mkutano huo unatarajiwa kumchaguwa mwenyekiti wake mpya ambapo Kansela Merz anatafuta uungwaji mkono wa kurejea kukiongoza chama hicho.Wabunge vijana wa Ujerumani watikisa siasa
Mkutano huo unafuatiliwa kwa karibu nchini Ujerumani na hasa kuona ni kwa kiasi gani Merz atakafanikiwa kuungwa mkono.
Mkutano huo wa siku mbili umekuja wakati ukiwa ni mwanzo wa mwaka wa hekaheka za uchaguzi kwa chama hicho cha CDU huku majimbo matano yakitarajia kufanya chaguzi zake ikiwa ni pamoja na jimbo la Baden- Wurttemberg litakaloanza uchaguzi mwanzoni mwa mwezi Machi.