1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa Democratic kuanza

19 Agosti 2024

Mkutano mkuu wa chama cha Democratic nchini Marekani unaanza mjini Chicago ukihudhuriwa na takribani wanachama 50,000, miongoni mwao ni maelfu ya wanaharakati wanaopanga kuandamana kupinga vita vya Gaza.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris (kulia), akiwa na mumewe Doug Emhoff.
Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris (kulia), akiwa na mumewe Doug Emhoff.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Mkutano huu wa siku nne unaoanza Jumatatu (Agosti 19), ni kilele cha safari ya takribani mwezi mmoja ya chama cha Democratic kuchaguwa mbadala wa Joe Biden kwenye kuwania kiti cha urais, kupambana na Donald Trump wa Republican, huku maoni ya wapigakura yakionesha kuwa wawili hao wanachuana vikali kuelekea tarehe4 Novemba

Wademocrat wanafunguwa mkutano wa leo wakiwa na mchanganyiko wa furaha na fadhaa kutokana na uamuzi wa dakika za mwisho wa kumchukuwa Kamala kuwa mgombea wao, kufuatia kujienguwa kwa Biden, ambaye tayari alikuwa amepitwa kwenye kura za maoni na Trump.

Soma zaidi: Mkutano Mkuu wa chama cha Democratic Marekani kuanza Jumatatu

Ingawa mapema mwezi huu, wajumbe wa Democratic waliridhia Kamala kuwa mgombea wao kupitia kura ya njia ya mtandao, lakini bado mkutano wa leo ni muhimu kwani unachukuliwa kama igizo la kura halisi na ya moja kwa moja, ambapo kawaida wajumbe hutangaza kura zao wakiwa ukumbini. 

Maandamano ya Gaza

Chama cha Democratic kinajaribu kujitambulisha kama chama kilichobadilika baada ya uteuzi huo wa Kamala, huku kiwango cha uungwaji mkono kifedha na wafuasi kwenye mikutano yao ya kampeni kikipanda juu, mbele ya kile cha Republican na mgombea wao, Trump.

Bango lenye picha ya Kamala Harris kwenye mkutano mkuu wa chama chake, Chicago.Picha: CHARLY TRIBALLEAU/AFP/Getty Images

Hata hivyo, mkutano huu unakabiliwa na maandamano makubwa ya wanaharakati wanaopinga vita, ambao wameapa kutuma ujumbe wa wazi kwa chama cha Democratic wanachokituhumu kuwaacha mkono watu wa Gaza na kumshutumu Rais Biden kuwa mshirika wa kile wanachokiita "mauaji ya kimbari ya watoto na wanawake wa Palestina."

Soma zaidi: Harris apendekeza juu ya namna ya kupunguza gharama za vyakula, nyumba

Chicago ni miongoni mwa miji ambayo ina idadi kubwa ya wakaazi wenye asili ya Kiarabu na Kiislamu, na kumekuwa kukifanyika maandamano ya mara kwa mara kuitaka Marekani kuacha kuisaidia Israel kwenye vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Biden ashitakiwa Congress

Hayo yakijiri, wajumbe wa Republican kwenye Baraza la Congress wamewasilisha kesi rasmi hivi leo ya kumuondoa madarakani Rais Joe Biden, wakimtuhumu kutumia vibaya ofisi yake. 

Wafuasi wa Kamala Harris wakimngojea kwa hamu kwenye uwanja wa ndege wa Pittsburgh, Pennsylvania.Picha: Brent Gudenschwager/ZUMA Press Wire/picture alliance

Ripoti ya kamati tatu zenye nguvu zinazoongozwa na Republican kwenye Baraza la Wawakilishi inamtuhumu Biden kwa ufisadi unaohusishwa na biashara za nje za mtoto wake wa kiume, Hunter Biden.

Soma zaidi: Trump aikosoa serikali ya Biden, huku akiahidi kuboresha hali ya Wamarekani

Jim Jordan, mkuu wa kamati ya masuala ya sheria, amesema kesi yao inaonesha kwa uwazi kabisa kwamba Biden alitumia vibaya ofisi ya umma kwa maslahi binafsi ya kifamilia na washirika wa biashara wa Hunter Biden.

Hata hivyo, mkururo wa hatua za kuchukuliwa kabla ya kesi hiyo kupata mashiko bungeni huenda usikamilike kabla ya Biden kumaliza muda wake madarakani na wengi wanaamini kesi hii ni kisasi tu kwa uamuzi wa Democrat kumshitaki mara mbili Trump alipokuwa madarakani. 

Chanzo: AP, Reuters