1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano Mkuu wa EU kuisadia Uingereza kuhusu Brexit

15 Oktoba 2017

Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kuweka mambo sawa na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wakati wa mkutano wa kilele mjini Brussels wiki hii, katika juhudi za kuondoa mkwano katika mazungumzo ya Brexit.

EU Gipfel Emmanuel Macron Angela Merkel und Theresa May
Picha: Reuters/F. Lenoir

Viongozi hao wa Ulaya watatangaza kuwa hakujakuwepo na hatua za msingi kuhusu masuala ya kutengana kwa pande hizo mbili, ikwemo ukubwa wa kiwango cha fedha inazopasa kulipa Uingereza kama gharama za kujitoa, ili kuwezesha kwenda katika hatua nyingine ya mazungumzo ya biashara, hadi kufikia alau mwezi Desemba.

Lakini katika ishara ya nia njema kwa kiongozi wa Uingereza aliedhoofishwa vibaya, wanapanga kusema kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kuanza maadalizi ya ndani ya mazungumzo kuhusu uhusiano wa baadae na Uingereza, ambayo itaondoka katika kanda hiyo ndani ya miezi 18 ijayo.

"Lengo ni kusaidia kidogo, kuionyesha London kwamba mlango haujafungwa kabisaa," duru moja ya kidiplomasia kutoka Umoja wa Ulaya ililiambia shirika la habari la Ufaransa AFP. "Lakini kimsingi hili halibadilishi chochote."

Majadiliano yamekuwa yakizidi kuwa ya hasira, huku Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker alisema siku ya Ijumaa kuwa "Waingereza laazima walipe" na waziri wa fedha wa Uingereza Philip Hammond akiutaja Umoja wa Ulaya kuwa "maadui".

Waziri Mkuu wa Ubelgiji Charles Michel, katika mahojiano yaliochapishwa siku ya Jumamosi, aliihimiza serikali ya May "kuafikiana miongoni mwao haraka iwezekanvyo" na kutatua migawanyiko kuhusu sera ya Brexit.

Waziri Mkuu Theresa May akiwa na Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk mjini London.Picha: Reuters/H. McKay

Agenda za Mkutono wa Kilele

Hali ya uhasama haipo tu katika mazungumzo -- harufu yenye kudhuru katika jengo la Europa ambako mkutano huo wa kilele unatarajiwa kufanyika iliwasababisha ugonjwa watu 20 siku ya Ijumaa na jengo hilo halitafunguliwa hadi siku ya Jumatatu.

Viongozi wote 28 wa kitaifa watakutana siku ya Alhamisi mjini Brussels kujadili ratiba ya mwenyeji wa mkutano huo ambaye pia ni rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk, kuhusu mustakabali wa Ulaya baada ya Brexit, huku mgogoro wa jimbo la Catalonia ukitarajia kuwa tu miongoni mwa mengineyo, na uhusiano kati ya umoja huo na Uturuki ukijadaliwa.

May kisha ataomba kuondoka baada ya kifungua kinywa siku ya Ijumaa ili viongozi wengine 27 wawezi kufikiria kwa makini kuhusu Brexit. Ujerumani inaongoza kundi la mataifa ya Umoja wa Ulaya yanayotaka suala nyeti la wajibu wa kifedha wa Uingereza kwa Umoja wa Ulaya kutatuliwa kabla ya majadiliano kufunguliwa kuhusu makubaliano ya bishara ya Brexit.

Wengine wanataka kuipa Uingereza kitu cha kujishikiza wakati kukiwa na hofu kwamba uwezekano wa hatari kwa uchumi - kuondoka bila makubaliano ifikapo Machi 29, 2019 unazidi kuwa mkubwa.

"Kuna aina mbili za mataifa ya Ulaya, yale yanayokosa usingizi kwa kufikiria kuhusu Brexit, na yale yaliojali," alisema mwanadiplomasia mwingine wa EU.

Masuala makuu yanayozusha sintofahamu

Umoja wa Ulaya unataka hatua kuhusu masuala matatu ya kutengana -- bili ya kutengana, haki za raia milioni tatu wanaoishi Uingereza na hatma ya Iralend ya Kaskazini na mpaka wake wa nchi kavu na mwanachama wa EU Iraland -- kabla ya kuendelea na mazungumzo ya biashara, kama inavyotaka Uingereza.

Kiongozi wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier alionya wakati wa duru ya mwisho ya mazungumz kati ya EU na UK kwamba majadiliano yalikuwa yamekwama kuhusiana na bili, ambayo EU inasema ni euro bilioni 100 wakati Uingereza inasema ni euro bilioni 20.

Mswada wa tamko la Mkutano Mkuu ambalo AFP ilipata nakala yake linasema wakati kuna "maendeleo", lakini hayatosi kunazisha awamu nyingine ya mazungumzo, na kubainisha kuwa kunakosekana dhamira thabiti na ya dhati kutoka kwa Uingereza kuhusu fedha.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker.Picha: imago/D.Shamkin

Watatathimini tena mwezi Desemba iwapo wahamie kwenye biashara, na kwa hivyo kuwa tayari kikamilifu kwa hilo wanampa mamlaka Barnier na nchi wanachama "kuanza mazungumzo ya matayarisho ya ndani."

Duru za Umoja wa Ulaya zilipuuza uvumi wa mtafaruku kati ya Barnier, ambaye anaripotiwa kutaka kuipa Uingereza kitu cha kuihimiza, na nchi wanachama zinazosita.

Askari mbaya, Askari mzuri

"Barnier na EU 27 wanabadilishana zamu za kucheza mchezo wa Askari mzuri, Askari mbaya," ilisema duru ya kidiplomasia. Sehemu kubwa ya mkutano lakini itaelekezwa kwenye mipango ya kuimarisha Umoja wa Ulaya baada ya mshtuko wa Brexit, mgogoro wa madeni wa kanda ya Euro na mgogoro wa wakimbizi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Juncker wote wamezindua hivi karibuni mikakakti yao ya wakati wa baadae, na Tusk ataainisha katika mkutano huo mipango yake ya utekekelezaji wa mikakati hiyo katika kipindi cha miaka miwili ijayo, hadi kwenye mkutano maalumu wa kilele nchini Romania, siku baada ya Uingereza kuondoka.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema Jumamosi kuwa waziri huyo mkuu wa zamani wa Poland ataeleza "namna tunavyoweza kuboresha mifumo yetu ya ufanyaji kazi na kuonyesha matokeo haraka."

Viongozi wa Umoja wa Ulaya huenda pia wakajadili msimamo mkali wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran ya 2015, uliozipelekea Ufaransa, Ujerumani na uingereza kutoa tamko kali Ijumaa, katika ishara kwamba ushirikiano kuhusu usalama na diplomasia unaendelea licha ya uhasama kuhusu Brexit.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri: Yusra Buwayhid

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW