1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mrefu wa mazingira wa UN wamalizika bila makubaliano

Sekione Kitojo
15 Desemba 2019

Mazungumzo marefu ya kimataifa ya mazingira yalifikia  mwisho leo Jumapili(15.12.2019) ambapo wajumbe wa majadiliano wameahirisha hadi mwakani maamuzi muhimu juu ya masoko ya gesi zinazoharibu mazingira duniani.

UN-Klimakonferenz 2019 | Cop25 in Madrid, Spanien | Carolina Schmidt, Cop25-Präsidentin
Picha: Getty Images/AFP/O. del Pozo

Baada  ya  wiki  mbili za  majadiliano  kwa lengo la  kupambana  na ongezeko la joto duniani, wajumbe  kutoka  karibu  mataifa  200 walipitisha  maazimio yanayotoa wito wa  kuongeza dhamira  kubwa  zaidi ya kupunguza gesi zinazosababisha sayari yetu kupata  joto  zaidi  na kuyasaidia  mataifa  masikini  yanayoathirika  na  athari  za mabadiliko  ya  tabia  nchi.

Wajumbe wa China katika mkutano wa Mazingira mjini Madrid COP 25Picha: Reuters/N. Doce

Lakini  licha  ya  kufanya  mazungumzo marefu  ya  mazingira  kuwahi kufanyika  katika  karibu  mikutano  25  ya  kila  mwaka, wajumbe wanaondoka  wakiwa  wameacha  masuala muhimu hadi  mkutano ujao  mjini  Glasgow, mwaka  mmoja ujao.

Makundi  ya  utetezi  wa  mazingira  pamoja  na  wanaharakati wameyashutumu  mataifa tajiri kwa  kuonesha  dhamira ndogo ya kupambana  kwa  dhati  na  mabadiliko  ya  tabia  nchi.

Masoko ya  gesi za  kaboni yameweka  bei kwa  utoaji wa  gesi  za kaboni dayoksaidi, gesi ambayo  inaharibu  mazingira, na  kuruhusu mataifa  ama  makampuni kuuza utoaji wa gesi hizo ambazo zinaweza taratibu  kupunguzwa, na  kuhimiza matumizi ya  teknolojia  zinazotoa gesi  hizo  chafu kwa  kiwango  kidogo.

Waziri wa mazingira wa Chile na rais mkutano wa mazingira wa Umoja wa mataifa COP 25 mjini Madrid Carolina Schmidt akihutubia Picha: Getty Images/AFP/O. del Pozo

Mataifa  ya  Ulaya  na  kwingineko yamesema  kuwa  kukosekana kwa  makubaliano  juu  ya  kushughulikia  mabadilishano ya mikopo ya  gesi za  kaboni ni  bora kuliko  kuwa  na  makubaliano  dhaifu ambayo  yanaweza  kudhoofisha  taratibu dazeni kadhaa  ama  zaidi zilizopo kikanda.

Maandamano ya hasira

"Kwa bahati  nzuri, sheria  dhaifu katika  soko chini  ya  misingi ya utaratibu, unaopigiwa  upatu na  Brazil na  Australia, ambao ungedhoofisha  juhudi  za  kupunguza utoaji  wa  gesi  hizo  chafu, umewekwa  kando,"  amesema  Mohamed Ado, mkurugenzi  wa Power Shift Africa, kundi linalofanya  kampeni.

Mazungumzo  kwa  wakati  fulani  yaliandamana  na maandamano ya hasira kutoka  kwa  makundi ya  watu wa asili na makundi ya mazingira, ndani  na  nje ya  ukumbi  wa mkutano. Waandamanaji wameakisi hali ya  kukata  tamaa inayoendelea, hususan miongoni mwa  vijana, kuhusu kasi ndogo  sana ya  juhudi  za  serikali kuzuwia mabadiliko  ya  tabia  nchi.

Miongoni mwa nyaraka  ambazo mkutano  huo wa  Umoja  wa mataifa umepitisha  leo Jumapili (15.12.2019) ni azimio  la  "Muda wa kuchukua  hatua Chile-Madrid" likitoa   mwito wa  mataifa  kuimarisha ahadi  zao  za  hivi  sasa za  kupunguza  utoaji  wa  gesi zinazoharibu  mazingira. Hii inahitajika  kuwa  katika  msitari  pamoja na  malengo  ya  makubaliano  ya  Paris ya 2015 ya  kuepuka ongezeko  la  nyuzi  joto  zaidi ya  1.5 'Celsius'  ifikapo mwishoni mwa  karne hii.

Mjumbe kutoka Brazil akinyanyua juu kibao cha nchi yake wakati wa majadilianoPicha: Reuters/N. Doce

Hadi sasa, dunia  imo  njiani  kufikia  ongezeko  la  nyuzi joto 3 hadi 4, kukiwa  na  uwezekano wa  matokeo  mabaya  zaidi  kwa  nchi nyingi.

Mataifa  pia  yamekubaliana  kuweka   fedha  kwa  mataifa  ambayo yamo  katika hatari  zaidi  na  yasiyo  na  uwezo kuwapa  fidia  kwa ajili  ya athari  za  matukio  ya  hali  mbaya  ya  hewa, moja kati ya masuala ya  dharura  zaidi  kwa  mataifa  madogo ya  visiwani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW