Mkutano ujao wa BRICS huenda ukafanyika Urusi
23 Agosti 2023Kwenye hotuba yake iliyorushwa kwa njia ya video katika ukumbi wa mikutano jijini Johannesburg, Putin aliwaalika wawakilishi wa mataifa mengine wanachama wa BRICS: Brazil, India, China na mwenyeji wa mara hii, Afrika Kusini, kwenye mji wa Kazan mwezi Oktoba mwakani.
Ingawa tarehe mahsusi haijatajwa, Putin alitangaza kwamba kutakuwa na matukio zaidi ya 200 ya kisiasa, kiuchumi na kijamii chini ya uwenyekiti wa nchi yake kwa BRICS mwaka ujao. Mkutano wa mwaka huu unamalizika kesho Alkhamis.
Waranti ya kukamatwa Putin
Hati ya kumkamata Putin iliyotolewa na Mahakama ya ICC kwa shutuma za kuhusika na uhalifu nchini Ukraine inamaanisha kuwa kiongozi huyo angekabiliwa na uwezekano wa kukamatwa lau angelihudhuria mkutano nchini Afrika Kusini, kwani nchi hiyo ni mwanachama wa ICC.
Rais Xi Jinping wa China, Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wanahudhuria wenyewe mkutano huo wa kilele.
Mjadala wa leo ulijikita kwenye jinsi jumuiya hiyo inavyoweza kuwasajili wanachama wapya wakati huu ikijipambanuwa kama taasisi ya kilimwengu mbali ya zile zinazodhibitiwa na mataifa ya Magharibi.
China, ambayo ndiyo yenye uchumi mkubwa zaidi kwenye umoja huo, inataka kuandikisha wanachama wapya kuharakishwe wakati huu ushindani na Marekani ukizidi.
Tayari mataifa 40 yamejipanga yakingojea kusajiliwa kuwa wanachama wa BRICS, lakini kwa sasa kikwazo kikubwa ni India, mwanachama mwengine mwenye nguvu, ndiyo yenye wasiwasi na kutanuka haraka kwa jumuiya hiyo.
Soma hii pia: Mkutano wa jumuiya ya BRICS waanza mjini Johannesburg
New Delhi inaamini kuwa Beijing inapigania kutanuka kwa BRICS ili kutanuwa himaya yake binafsi ya kiuchumi duniani kwa kutumia mgongo wa jumuiya hiyo.
Brazil na Afrika Kusini zinaunga mkono utanukaji huo, ambapo Rais Lula da Silva wa Brazil amesema yuko tayari kuipokea Argentina.
Mataifa mengine yaliyo mbioni kujiunga ni Saudi Arabia, Algeria, Ethiopia na Iran.
Asilimia 40 ya watu wote waliopo ulmwenguni wanaishi sasa kwenye mataifa matano waanzilishi wa BRICS, ambayo kwa pamoja yanahodhi robo nzima ya uchumi wa dunia.Afrika Kusini na China zina maoni sawa kuitanua BRICS
Lengo la kutanuwa uwanachama ni kuiruhusu jumuiya hiyo kuyaleta pamoja mataifa yenye chumi kubwa ama ndogo, yenye serikali za kidemokrasia ama kidikteta ili kujenga chombo mbadala kinachofuata utaratibu tafauti wa kilimwengu na ule uliowekwa na kusimamiwa na mataifa ya Magharibi.
Vyanzo: dpa, AFP