1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano usio wa G-8 Mali

10 Julai 2008

Mkutano wa wakereketwa mali unaopingana na ule wa G-8 uliofanyika Japan.

Baada ya kikao cha siku 3,mkutano wa kilele wa nchi 8-tajiri kabisa duniani-(G-8), ulimalizika jana nchini Japan.Mbali sana kutoka kituo cha mkutano wa dola hizo tajiri ulimwenguni,ulimalizika jana pia mkutano mwengine -ule wa "wanyonge" au wa "masikini wa sayari hii".Huko Mali, Afrika magharibi,mojawapo ya nchi masikini kabisa duniani,walikutana kwa muda wa siku 4 wakereketwa mia kadhaa wanaoupinga mfumo wa kibepari wa utandawazi.

Kituo cha mkutano huu wa mafukara-KATIBOUGOU kipo km 50 mashariki mwa mji mkuu wa Mali-Bamako.Tangu miaka kadhaa iliopita mji huu mdogo uliojaa vumbi umegeuka shina la wakereketwa wa kiafrika wanaopinga mfumo wa utandawazi-globalisation.

Washiriki mkutanoni hutoka kila pembe ya Afrika ili kuelezea matatizo maalumu yanayowakabili na kuonesha njia gani zafaa kufuatwa tofauti kabisa na utandawazi.

Sawa na ilivyokua kwenye mkutano wa siku 3 huko Japan wa kundi la nchi-8 tajiri,kikao cha Katibougou,nchini Mali, kilijishughulisha na swali la upungufu wa chakula.Ukosefu wa chakula cha kutosha baranio Afrika ,wajumbe huko Katibougou wanatwika jukumu mabegani mwa mfumo wa uchumi wa kibepari ulitia fora duniani. Na hivyo,wanazilaumu nchi za kiviwanda.

Wanashauri kutegemea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kupunguzwe na mtindo wa kufidia bidhaa za nje upungue.Wakereketwa hao huko Mali , kwamba Afrika inaweza kujitosheleza yenyewe kwa chakula.Jinsi Afrika ilivyo na neema ya vyakula mbali mbali,soko maalumu pembezoni mwa kikao chao.

Katika kituo cha Taasisi ya kilimo cha mji huu wa Katibougou, ambacho kilijengwa kwa msaada wa Urusi,kuna mchanganyiko wa vyakula.Kuna vijiduka vya wauzaji mbazi na mchele,matunda kama embe au mazao ya pamba inayovunwa nchini.

Maendeleo ya Afrika waliadi wajumbe yasiachiliwe pekee mikononi mwa nchi za magharibi.Haifai kabisa kutegemea ahadi na vitita vya fedha kutoka nchi za viwanda za kaskazini mwa dunia hii-asema Solange Kone kutoka Ivory Coast.Anaongeza,

"Ningesema kutegemea misaada pekee hakutaliendeleza mbele bara letu.Ni wakaazi wake tu ndio watakaowezay kuhakikisha siku njema za usoni za bara lao.Na hapa ndipo ninapoona kundi letu hili linapochangia ."

alisema Kone anaewakilisha kikundi cha maendeleo ya jamii nchini I.Coast.

Katika mkutano wa Katibougou,Mali, shabaha ilikua kuonesha umoja na mshikamano miongoni mwa majirani barani Afrika.Lakini, licha kusisitizwa haja ya waafrika kujitwika jukumu la maendeleo yao wao binafsi,wakereketwa wengi waliuliza wakitupa jicho Japan : iwapi ile ahadi ya nchi hizo 8 tajiri kabisa ulimwenguni kutoa dala bilioni 25 hadi ifikapo 2010 kwa maendeleo ya viwanda ya Afrika ?

Hii ni ahadi ambayo nchi hizo za G-8 zilitoa katika kikao cha Gleaneagles,miaka 2 iliopita.kwani, hadi sasa ni dala bilioni 3 tu zilizotolewa kwa muujibu vile alivyoarifu mjumbe wa shirika la misaada la OXFAM mwanzoni mwa wiki hii.

Swali linaloulizwa : kwanini kundi la G-8 lashindwa kutekeleza ahadi zake ?

Doumanite Bao ni Katibu mkuu wa shirika la maendeleo nchini Mali (CAD) kwa ufupi ambalo ndilo lililoandaa mkutano huu unaopingana na ule wa G-8 nchini Japan.

Aonavyo yeye ni wazi kabisa.Wanasiasa wa nchi zilizoendelea kiviwanda hawana nia kweli ya kulisaidia bara la Afrika. Anadai:

"Hazitaki kuikomboa Afrika kujitoa kwenye misukosuko yake.Uchambuzi wote unabainisha ,mfumo wa nchi za Afrika kuingia kwenye madeni na kulipa madeni hayo unatunasa katika mtego mbaya sana.Unaongoza kunyonywa mali zetu za asili kwa masilahi ya nchi za kiviwanda.Bara letu si masikini,bali ni bara linalofanywa kuwa masikini."-alisema Doumanite Bao kutoka Mali.