Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika wafunguliwa Addis Ababa
14 Februari 2026
Wakuu wa nchi na serikali wa nchi za Afrika wanakutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa tarehe 14 na 15 Februari kwa ajili ya Kikao hicho cha 39 cha Baraza la Umoja wa Afrika (AU) kilichoanzia tarehe 11 Februari.
Burundi imepangiwa kuchukua nafasi ya uenyekiti huku rais Evariste Ndayishimiye akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa AU kwa mwaka 2026.
Suala la maji kama rasilimali muhimu ndilo mada rasmi ya mkutano wa kilele wa mwaka huu. Akihutubia mkutano wa Baraza Kuu wiki hii, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf alisisitiza umuhimu wa rasilimali hiyo.
Kuongezeka kwa hali ya sintofahamu duniani
Migogoro na usalama ni maswala yanayotarajiwa kuwa ajenda kuu ya mkutano huo wa kilele. Mkutano huo unafanyika wakati ambapo migawanyiko ya kimataifa inaongezeka, ushirikiano wa pande nyingi, ukiendelea kupungua, dunia inakabiliwa na kuongezeka kwa migogoro, kuongezeka kwa dhiki ya madeni, na kuongezeka kwa shinikizo linalotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya AU. Mahmoud Ali Youssouf, alikutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika huko mjini Addis Ababa kujadili juu ya kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi wakati hali ya kutokuwepo na uhakika duniani ikiendelea kuongezeka.
Jitihada za kutatua mizozo
Mbali na migogoro inayoendelea Sudan, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, eneo la Sahel na migogoro iliyoibuka upya ya Sudan Kusini, Libya na Ethiopia, msemaji wa Halmashauri ya Jumuiya ya Umoja wa Afrika Nuur Mohamud Sheekh, aliwaambia waandishi wa habari kwamba AU imesaidia kupunguza mivutano ya kisiasa na kutoa usaidizi kabla ya hali kugeuka na kuwa vurugu, akitoa mfano wa kazi iliyofanywa kuzuia vita kati ya Sudan na Sudan Kusini kuhusu eneo la Abiyei.
Donald Trump hahudhurii mkutano wa Umoja wa Afrika lakini...
Bila kuhudhuria, kiwingu cha rais wa Marekani Donald Trump kimeghubika chumba cha wakati mkutano huu wa kilele wa 39 wa Umoja wa Afrika.
Sera zake kuhusu ushuru, misaada ya kigeni na uhamiaji zimesababisha athari kubwa huku viongozi wa Afrika wakitafuta usawa. Katikati ya msukosuko huo, utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umejitahidi kufikia makubaliano mapya ya pande mbili na nchi za Afrika, yanayolenga kupata faida za rasilimali za Afrika na usalama kwa Marekani.
Katika Mazungumzo ya Ngazi ya Juu kuhusu "Jukumu la sekta binafsi katika kufanikisha Ajenda ya Afrika ya 2063” kandoni mwa Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika (AU) huko Addis Ababa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya AU. Mahmoud Ali Youssouf, alisisitiza: "Kipindi cha Afrika cha kusafirisha malighafi na kuagiza bidhaa zenye thamani lazima kimalizike”.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika amesema kwa watu bilioni 1.4, barani Afrika asilimia 30 ya madini muhimu duniani na na kwa kuzingatia Mkataba wa Biashara Huria wa Bara la Afrika AfCFTA ukiwa kama msingi, rasilimali za bara hilo zinaweza kustawisha viwanda, kuunganisha, na kuongoza. Amesema sera ya umma pekee haitoshi bali Afrika inahitaji ushirikiano kamili wa sekta binafsi na viwanda, mpito wa nishati, uvumbuzi wa kidijitali, na maendeleo ya mnyororo wa thamani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf, amesisitiza kwamba AU itaimarisha mshikamano wa kisheria, kupunguza vikwazo visivyo vya ushuru, na kuzindua Mfumo wa Kudumu kwa ajili ya mazungumzo ya kimkakati na biashara yanayozingatia matokeo barani Afrika na alimalizia kwa kusisitza kuwa "kila kazi ni mchango wa amani, kila uwekezaji ni kura ya imani kwa mustakabali wa Afrika."